1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Mateso ya Taliban kwa wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinadamu

John Juma
26 Mei 2023

Mashirika ya haki za binadamu yamelishutumu Taliban kwa kuwawekea wanawake na wasichana vikwazo vikali. Mashirika hayo yamevitaja vikwazo hivyo kama mateso ya kijinsia ambayo ni 'uhalifu dhidi ya ubinadamu'.

https://p.dw.com/p/4Rqap
Afghanistan Taliban Frauen Burka Essensverteilung
Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Kwenye ripoti mpya, shirika la Amnesty International na Tume ya Kimataifa ya Wanasheria au ICJ, yalisisitiza jinsi ukandamizaji wa Taliban dhidi ya haki za wanawake pamoja na vifungo gerezani, watu kupotezwa kwa lazima, mateso na dhuluma nyinginezo, vinaweza kuzingatiwa kama mateso ya kijinsia chini ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.

Ripoti hiyo yenye kichwa: "Vita vya Taliban dhidi ya Wanawake, Uhalifu dhidi ya Ubinadamu na mateso Afghanistan" ilitaja sheria ya mahakama ya ICC inayoorodhesha unyanyasaji wa kijinsia kama uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Afghanistan yajadiliwa kimataifa

Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International, ameitaka jamii ya kimtaifa kuuvunja ule aliosema ni "mfumo wa ukandamizaji na mateso wa kijinsia", huku akisisitiza kuwa yanayofanyika Afghanistan ni vita dhidi ya wanawake.

Amnesty International pia ilitaja visa vya wanawake na wasichana kuozeshwa kwa lazima kwa wanachama wa Taliban.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalishutumu kundi la Taliban kwa kuhujumu haki za wasichana na wanawake wa Afghanistan ikiwemo vikwazo dhidi yao kupata elimu na kazi na vilevile kuwaoza baadhi yao kwa lazima.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalishutumu kundi la Taliban kwa kuhujumu haki za wasichana na wanawake wa Afghanistan ikiwemo vikwazo dhidi yao kupata elimu na kazi na vilevile kuwaoza baadhi yao kwa lazima.Picha: Ximena Borrazas/ZUMA Wire/IMAGO

ACJ_ Vita vya Taliban vinaingia kwenye kundi la uhalifu dhidi ya ubinadamu

Santiago A. Canton, Katibu Mkuu wa shirika la ICJ, amesema vitendo vya Taliban vinatekelezwa kwa ‘wingi na utaratibu' na kwamba "vinaingia kwenye kundi la uhalifu dhidi ya ubinadamu hasa unyanyasaji wa kijinsia."

Mataifa yajadili haki za wanawake wa Afghanistan

Mashirika hayo yametoa wito kwa nchi pia kuliwajibisha kundi la Taliban chini ya sheria ya kimataifa.

Ripoti hiyo pia imelituhumu kundi la Taliban kwa kuwalenga wanawake na wasichana walioshiriki maandamano ya amani na kuwafunga jela au kuwapoteza kwa lazima na kuwatesa wakiwa vizuizini. Ripoti imeongeza kuwa kundi la Taliban pia limewalazimisha wale waliokamatwa kusaini ahadi za kiapo kwamba hawataandamana tena.

Kundi la Taliban lilichukua madaraka nchini Afghanistan Agosti 2021, wakati majeshi ya Marekani na ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO yalipojiondoa nchini humo baada ya miongo miwili ya vita.

Waandamanaji mjini Berlin Ujerumani kulaani dhuluma dhidi ya wasichana na wanawake zinazofanywa na Taliban nchini Afghanistan.
Waandamanaji mjini Berlin Ujerumani kulaani dhuluma dhidi ya wasichana na wanawake zinazofanywa na Taliban nchini Afghanistan.Picha: Olaf Schuelke/IMAGO

Taliban na tafsiri yake ya Sharia

Licha ya ahadi za awali za kutekeleza sheria za kawaida, utawala wa Taliban ulianza kuweka vikwazo dhidi ya wanawake na wasichana, kuwazuia kushika nyadhifa na kazi nyingi za umma.

Umoja wa Mataifa walaani Taliban "kuwakandamiza" wanawake

Aidha kundi hilo liliwapiga marufuku wasichana kupata elimu ya zaidi ya darasa la sita. Hatua hizo zilirejesha misimamo ya utawala uliopita wa Taliban nchini Afghanistan, mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati walipoweka tafsiri yao kali ya sheria za dini ya Kiislamu au Sharia.

Sheria hizo kali zilizusha shutuma za kimataifa dhidi ya Taliban, ambao utawala wake haujatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa.
(Chanzo: APAE)

Meza ya Duara: Shinikizo la kimataifa kwa utawala wa Taliban