Mashambulizi yazidi Katika Ukanda wa Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mashambulizi yazidi Katika Ukanda wa Gaza

Mtoto mmoja ameuwawa huku watu wengine 30 wakijeruhiwa baada ya roketi kuvurumishwa katika kambi ya wakimbizi ndani ya Ukanda wa Gaza, dakika chache baada ya Irael kutangaza kusitisha mapigano kwa masaa saba.

Wanajeshi wa Israel wakirusha kombora katika Ukanda wa Gaza

Wanajeshi wa Israel wakirusha kombora katika Ukanda wa Gaza

Msemaji wa huduma za dharura wa Palestina amesema roketi lilipiga kambi hiyo ya wakimbizi ya Shati na kumuua mtoto mmoja wa kike aliye na umri wa miaka minane, na kwamba wengi waliojeruhiwa ni wanawake na watoto.

Walioshuhudia wanasema shambulizi hilo lilitokea upande wa Israel, lakini hapajakuwepo na tamko lolote juu ya shambulizi hili kotoka jeshi la Israel lililosema bado linaangalia habari hiyo kwa undani zaidi.

Mapema hii leo Israel ilitangaza kusitisha mapigano kwa takriban masaa saba ili kutoa nafasi kwa misaada ya kiutu kuingia katika maeneo yalioathirika lakini ikasema bado itaendelea na operesheni yake ya kuyaharibu mahandaki yanayotumiwa na wanamgambo wa Hamas kulishambulia taifa hilo la Kiyahudi.

Wanamgambo wa Hamas

Wanamgambo wa Hamas

Balozi wa Israel nchini Marekani Ron Dermer wasichokitaka ni kutoa nafasi kwa Hamas kujihami na kuchimba mahandaki zaidi.

Masaa chache baada ya mashambulizi ya leo, kundi la Kiislamu la Lihadi lililo mshirika wa karibu wa Hamas lilisema kamanda wake, Daniel Mansour, ameuwawa baada ya roketi kutoka Israel kulenga nyumba yake. Awali msemaji wa Hamas, Sami Abu Zuhri aliwaonya raia wa Palestina kuchukua tahadhari akisema kuwa haamini tamko la Israel la kusimamisha mapigano kutokana na ahadi kama hizo kuvunjwa.

Idadi ya Waplestina waliouwawa yazidi kuongezeka

Tangu Israel ilipoanzisha hujuma yake katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kupambana na wanamgamo wa Hamas, zaidi ya Wapalestina 1,700 wameuwawa wengi wao wanawake na watoto huku Israel nayo ikipoteza wanajeshi 64 wakiwemo raia wawili.

Huku hayo yakiarifiwa, wawakilishi wa Hamas na wenzao wapiganaji wa Jihadi wanaendelea na juhudi za kidiplomasia za kusimamisha mapigano zinazoongozwa na Misri. Israel imekataa kuhudhuria mkutano huo unaofanyika mjini Cairo.

Huku makombora yakiendelea kuvurumishwa katika Ukanda wa Gaza, bado viongozi mbalimbali duniani wameendelea kulaani mauaji yanayoendelea katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Mtu aliyejeruhiwa akimbizwa kwa matibabu

Mtu aliyejeruhiwa akimbizwa kwa matibabu

Marekani imesema imesikitishwa na yale yanayoendelea na kumuhimiza mshirika wake wa karibu, Israel, kufanya kila iwezalo ili kuepuka mauaji ya raia katika vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hamas ambao Marekani imewaorodhesha kama magaidi.

Umoja wa Ulaya ulio na nchi wanachama 28 umesema katika taarifa yake iliyotiwa saini na rais wa Halmashauri ya Umoja huo, Jose Maneul Barroso, kuwa unazihimiza pande zinazohasimiana kukomesha mara moja uhasama wao katika Ukanda huo Gaza.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com