1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaendelea Gaza huku mazungumzo yakianza Cairo

31 Machi 2024

Mashambulizi makali ya angani yameupiga Ukanda wa Gaza usiku kucha wakati mazungumzo ya kusitishwa mapigano kati ya Israel na Hamas yakitarajiwa kuanza tena mjini Cairo Jumapili.

https://p.dw.com/p/4eIBW
Mashambulizi Gaza
Israel imeendeleza mashambulizi ya usiku kucha katika Ukanda wa Gaza na kuharibu majengoPicha: AFP

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas watu 75 waliauwa usiku kucha katika mashambulizi mapya ya Israel, wengi wao wanawake na watoto. Mashambulizi ya makombora yamerindima katika mitaa ya Ukanda huo uliozingirwa na Israel.

Ili kusaidia kupunguza mateso ya wakazi milioni 2.4 wa Gaza, meli nyingine ya msaada iko njiani kutoka taifa la kisiwa la Cyprus katika bahari ya Mediterania kupeleka tani 400 za msaada wa chakula.

Akikabiliwa na shinikizo kubwa la kuwaleta mateka nyumbani, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliidhinisha Ijumaa duru mpya ya mazungumzo ya kusitishwa mapigano kufanyika Doha na Cairo.

Televisheni ya Al-Qahera nchini Misri, ambayo ina uhusiano wa karibu na vyombo vya intelijensia vya nchi hiyo, imesema mazungumzo yataanza tena Jumapili.

Netanyahu yuko chini ya shinikizo kutoka kwa jamaa za mateka na wafuasi, ikiwemo maandamano makubwa ya Jumamosi usiku mjini Tel Aviv ambapo polisi walitumia mizinga ya maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji waliowachoma moto matairi na kuzifunga barabara kuu.