1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanzisha mashambulizi yake mjini Rafah

25 Aprili 2024

Maafisa wa hospitali ya Palestina wamesema mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Israel usiku kucha katika mji wa Kusini wa Rafah, yamewauwa watu watano miongoni mwao watoto wawili wadogo.

https://p.dw.com/p/4fB1Y
Mzozo wa Mashariki ya Kati
Israel imeanzisha mashambulizi katika mji wa Kusini wa Rafah, yaliosababisha mauaji ya watu watano wakiwemo watoto wawili wadogoPicha: Jack Guez/AFP

Kulingana na rekodi za hositali, miongoni mwa watu hao watano waliouwawa ni watoto wawili wadogo waliotambuliwa kama Sham Najjar, alliye na miaka sita na Jamal Nabahan, wa miaka minane. Zaidi ya nusu ya idadi ya watu katika ukanda wa Gaza ya milioni 2.3, wamekimbilia usalama wao katika mji huo wa kusini wa Gaza ambapo Israel imekuwa ikiuvamia mara kwa mara huku ikijitayarisha kushambulia kikamilifu.

Shambulizi jengine la Israel katika mji wa kati wa Gaza, lilisababisha mauaji ya watu wanne ambao miili yao baadae ilipelekwa katika hospitali iliokuwa karibu. Familia za watu hao ilisema waliuwawa walipokuwa wakijaribu kuingia kaskazini mwa Gaza ambapo wanajeshi wa Israel wanadaiwa kuwazuwia watu kurejea majumbani mwao.

Israel yafanya mashambulizi ya anga Gaza

Israel imeapa kutanua mashambulizi yake ya ardhini dhidi ya kundi la Hamas, ndani ya mji huo unaopakana na Misri licha ya miito chungu nzima kutolewa na washirika wake ikiwemo Marekani dhidi ya kuchukua hatua hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Khalil al-Hayya, ameliambia shirika la The Associated press kwamba kundi hilo liko tayari kufikia makubaliano ya amani ya miaka mitano au zaidi na Israel, kuweka chini silaha zake na kubadilika kuwa chama cha kisiasa, iwapo dola huru la Palestina litaundwa ikizingatiwa mipaka iliyowekwa mwaka 1967.

Hatua hiyo inasemekana kuwa muhimu, lakini Israel haitegemewi kukubaliana na mapendkezo hayo ikizingatiwa kuwa imeapa kulitokomeza kabisa kundi la Hamas na utawala uliopo sasa Israel, unapinga kabisa kuundwa kwa taifa la Palestina katika ardhi iliyonyakuliwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967.

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya Gaza

Matamshi ya Khalil al-Hayya yamekuja wakati mazungumzo ya kutafuta njia ya kukomesha vita kati ya mahasimu hao wawili Israel na Hamas yakikwama.

Gaza iko katika hatari ya kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula
Wapalestina wakionekana kukimbilia chakula cha msaada kilichodondoshwa kutoka angani kwa wakaazi hao wanaokabiliwa na vita.Picha: Mahmoud Issa/dpa/picture alliance

Kwengineko hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya kundi la Hamas. Hapo jana rais wa Marekani Joe Biden alitia saini sheria ya msaada wa kivita wa dola bilioni 95 ambapo dola bilioni 9 zitaelekezwa kwa Palestina kukabiliana na hali hiyo ya kibinaadamu inayozidi kuzorota.

Ujerumani kuanza tena ushirikiano na shirika la Palestina UNRWA

Vita hivyo vilianza mnamo Oktoba 7 wakati wanamgambo wa Hamas waliposhambulia kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 na kuwachukua mateka zaidi ya watu 200. Tangu wakati huo Israel ikaanzisha vita vyake dhidi ya kundi hilo katika ukanda wa Gaza ambapo hadi sasa vimesababisha mauaji ya zaidi ya wapalestina 34,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya ya Gaza.

Vita hivyo vimeisambaratisha miji miwili mikubwa ya Gaza na kuacha uharibifu mkubwa wa mali. Takriban asilimia 80 ya idadi ya watu imekimbili katika maeneo mengine ya pwani yanayozingirwa na wanajeshi wa Israel.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

afp/ap