Marufuku kuripoti ushuhuda wa waathiriwa wa ghasia Tanzania
26 Januari 2026
Tume huru ya uchunguzi wa vurugu za Oktoba 29 nchini Tanzania, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imezuia wanahabari kushiriki katika mahojiano yanayofanywa kati ya tume hiyo na waathirika wa vurugu za Oktoba 29, imedai kuwa kuchapishwa kwa taarifa zao kunachagiza msongo wa mawazo. Hata hivyo uamuzi huo umepokewa kwa mtazamo tofauti na wadau wa masuala ya Habari na wa afya ya akili Tanzania.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman na kaimu wake, Jaji Mstaafu Ibrahim Juma imetoa uamuzi huo juzi, Januari 24 ikisisitiza kuwa imechukua uamuzi wa kuzuia wanahabari wakati wa shuhuda za waathiriwa wa vurugu za oktoba 29 ili kulinda usalama na faragha za waathirika hao.
Kwa mujibu wa tume hiyo, hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuibuka kwa malalamiko kuwa taarifa binafsi za waathirika zinasambazwa mitandaoni bila ridhaa yao.
Madai ya waathiriwa kusumbuliwa na vyombo vya habari kwa mahojiano
Profesa Juma amebainisha kuwa kusambaa kwa taarifa hizo kumesababisha baadhi ya waathirika kusumbuliwa na maombi ya mahojiano kutoka kwa vyombo mbalimbali vya habari, jambo linalowaletea msongo wa mawazo na changamoto ndani ya familia zao.
Hata hivyo uamuzi wa tume hiyo umepokewa kwa mitazamo tofauti na wadau wa Habari, haki za binadamu na wanahabari, ambao wanautaja uamuzi huo kama unaoondosha mantiki ya tume huru na ya wazi.
Akizungumza na DW, Mchambuzi wa masuala ya Habari na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga amesema “Sijui kwa nini wamechukua uamuzi huo kwa sababu mambo yaliyotokea kipindi kile ni mambo yaliyokuwa hadharani. Kwa hiyo watu waliyaona, waliyaongelea, watu wanalalamika, na kadhalika. Nadhani ni salama kufikiria kwamba hata hiyo tume ikaundwa.”
Tume kutafuta chanzo cha vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29
Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume hiyo ili kutafuta chanzo cha vurugu za Oktoba 29 wakati wa uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi huo wa Tanzania na katika hotuba zake amekuwa akiisitiza kuwa tume hiyo ni huru na anaiamini.
Akizungumzia uamuzi wa tume hiyo na dhana ya waathirika kuathiriwa zaidi kisaikolojia, mtaalamu wa afya ya akili, Saldine Kimangale alisema: “Sio wanahabari pekee, hata yale mazungumzo, yanaweza kuchagiza kumbukumbu za zamani, za tukio lililotokea, si lazima iwe mwanahabari awe ameripoti.”
Tume hiyo imeshakamilisha kusikiliza waathirika katika wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, na Ubungo mkoani Dar es Salaam na inatarajiwa kuendelea na mikutano yake katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Ruvuma, na Iringa kukusanya taarifa za matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.