Mapigano makali yazuka Aleppo | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mapigano makali yazuka Aleppo

Mapigano makali yamezuka leo katika mji wa kaskazini wa Aleppo, ikiwa ni siku moja baada ya waasi kudhibiti kambi ya karibu ya jeshi. Aidha, mripuko uliosababisha mauaji umetokea katika mji wa Raqa.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Mapigano hayo makali kati ya waasi dhidi ya vikosi vya serikali, yametokea leo Jumatano karibu na jengo la kambi ya jeshi huko Layramun pembezoni mwa mji wa Aleppo. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa shirika la kusimamia haki za binaadamu la Syria.

Shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza limesema waasi walioshiriki katika mapigano hayo ni wa kutoka kwenye makundi ya Waislamu wenye itikadi kali, likiwemo kundi la Jihadi la Al-Nusra Front. Mapigano hayo yametokea ikiwa ni siku moja baada ya waasi kuidhibiti kambi ya karibu ya jeshi ya Minnigh.

Wanajeshi wa serikali ya Syria

Wanajeshi wa serikali ya Syria

Mwanaharakati mmoja aliyeko Aleppo, Mohammed amesema kuwa waasi walikuwa wanajaribu kuelekea kwenye vijiji vya Nabul na Zahraa, ambavyo vina wakaazi wengi wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia, ambavyo vimekuwa ngome ya serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Wengi wa waasi wa Syria ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni, huku Rais Assad akiwa anatokea katika jamii ya madhebu ya Alawi, yaliyotokana na Shia.

Mohammed ambaye ni mwanaharakati wa kituo cha habari kinachoipinga serikali, amesema kuwa kiasi wapiganaji 300 ambao wamekuwa wanapigana huko Minnigh sasa wako huru kupigana kokote kule.

Mripuko mwingine watokea Raqa

Ama kwa upande mwingine, mripuko mkubwa umetokea kaskazini mwa mji wa Raqa, na kuwaua watu watatu, wakiwemo watoto wawili.

Shirika la kusimamia haki za binaadamu la Syria, limesema kuwa chanzo cha mripuko huo ambao umesababisha watu kadhaa kujeruhiwa, bado hakijajulikana.

Waasi wa Syria

Waasi wa Syria

Aidha, karibu na mji mkuu wa Damascus, shambulizi lililofanywa na jeshi la Syria, limewaua kiasi waasi 62 na kuwajeruhi wengine karibu na mji wa viwanda wa Adra, ulioko kaskazini-mashariki mwa Damascus.

Eneo hilo limekuwa likishuhudia ghasia katika wakati ambapo waasi wanajaribu kuchukua udhibiti na kulifanya kama eneo la kuanzisha mashambulizi ndani ya Damascus.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa zaidi ya watu 100,000 wameuawa katika vita vya Syria na mamilioni wengine hawana makaazi.

Wachunguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa kuelekea Syria wiki ijayo

Katika hatua nyingine, timu ya wachunguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, waliopewa jukumu la kuchunguza madai kwamba silaha za kemikali zilitumika Syria, wanakamilisha maandalizi yao kuelekea Damascus.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky, amesema wanatarajia kukamilisha maandalizi yao mjini The Hague ndani ya siku chache zijazo na kwamba tarehe rasmi ya kuanza kwa safari yao itatangazwa badae.

Kiongozi wa timu ya wachunguzi wa UN, Ake Sellstrom

Kiongozi wa timu ya wachunguzi wa UN, Ake Sellstrom

Wachunguzi hao wanatarajiwa kuwepo Syria wiki ijayo na watakamilisha kazi yao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Timu hiyo ya wachunguzi wa umoja wa Mataifa, itakayoongozwa na mtaalamu kutoka Sweden, Ake Sellstrom, inatarajia kuchunguza maeneo matatu ambayo yameripotiwa kuwa silaha za kemikali zilitumika. Moja ya maeneo hayo ni Khan al-Assal na maeneo mengine mawili bado hayajatangazwa hadharani kwa sababu za kiusalama.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com