Waasi wa Syria kukwepa mkutano wa Geneva | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wa Syria kukwepa mkutano wa Geneva

Kiongozi mpya wa muungano wa waasi wa Syria, Ahmad Jarba (pichani juu) amesema muungano wao hautashiriki katika mazungumzo ya amani yaliyopendekezwa na Urusi na Marekani, hadi watakapoweza kujiimarisha tena kijeshi.

Ahmad Jarba, kiongozi mpya wa muungano wa waasi wa Syria

Ahmad Jarba, kiongozi mpya wa muungano wa waasi wa Syria

Kauli ya Ahmad Jarba kuhusu kutoshiriki kwa muungano wa waasi wa Syria katika mazungumzo ya amani yanayoandaliwa kwa ajili ya nchi hiyo, ilitolewa katika mahojiano yake ya kwanza na vyombo vya habari, baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa muungano huo, Jumamosi iliyopita.

Amesema kuwa muungano wao unategemea kupata msaada mkubwa wa silaha hivi karibuni.

'Mkutano wa Geneva hauwezekani katika hali ya sasa. Tunaweza kushiriki katika mkutano huo ikiwa tu tutahisi kama tuko imara kijeshi, tofauti na sasa ambapo tunajikuta katika hali dhaifu.' Alisema Ahmad Jarba.

Kiongozi huyo wa muungano wa waasi ambaye anaungwa mkono na Saudi Arabia, alisema silaha hizo watakazozipata zitabadilisha hali ya mambo kwenye uwanja wa vita.

Moto wazidi kuwapa Homs na Aleppo

Mapigano yameugeuza magofu mji wa Homs

Mapigano yameugeuza magofu mji wa Homs

Wakati Ahmad Jarba akiyatangaza hayo, mapigano makali yameendelea katika miji ya Homs na Aleppo. Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema kuwa mapambano baina ya jeshi la serikali na waasi yameangamiza takribani theluthi mbili za wilaya ya Khaldiyeh inayodhibitiwa na waasi.

Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman aliliambia shirika la habari la AFP kuwa maelfu ya wakazi wa mji huo ulio katikati mwa nchi wamekimbia. Rahman alisema kuwa hata ikiwa jeshi la serikali litafanikiwa kuuteka mji huo, nyumba zote zitakuwa zimebomolewa.

Waasi wakiri kubanwa

Mwanaharakati wa upinzani dhidi ya rais Assad, Abu Khaled amesema kuwa jeshi la serikali limekuwa likisonga mbele taratibu kuizingira wilaya ya Khaldieh, na kukiri kuwa wanajikuta chini ya shinikizo kubwa, kutokana na uhaba wa zana za kivita.

Waasi wa Syria wanasakamwa vikali na jeshi la serikali

Waasi wa Syria wanasakamwa vikali na jeshi la serikali

Hali pia ni ya wasiwasi mkubwa katika wa Aleppo, ambao ndio mkubwa zaidi nchini Syria. Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria limearifu kuwa risasi zilianguka katika gereza kuu la mji huo, na kuwauwa wafungwa sita. Hali kadhalika, shirika hilo lilisema kuwa wanajeshi na wapiganaji wapatao 70 waliuawa katika mapigano yaliyoendelea jana Jumapili, na kuongeza kuwa raia wasiopungua 40 pia walipoteza maisha yao katika makabiliano hayo.

Utata wilayani Khaldieh

Ripoti zilizotolewa na serikali hivi punde, zimedai kuwa tayari jeshi la serikali limechukua udhibiti kamili wa wilaya ya Khaldieh, na kwamba kinachoendelea sasa ni kile zilizokiita 'kusafisha' sehemu sehemu chache wanakosalia waasi. Hata hivyo ripoti hizo zimekanushwa na mwanaharakati wa upinzani ambaye alisema kuwa waasi bado wanaendelea kujizatiti katika wilaya hiyo, huku wakiwa wamelemewa.

Kutokana na operesheni kubwa ambazo serikali imeianzisha dhidi ya waasi, udugu wa kiislamu nchini Syria umeziomba nchi za magharibi kuwapa waasi msaada wa haraka, na kuongeza kuwa umekatishwa tamaa na jinsi nchi hizo zinavyosuasua katika kuwasaidia waasi.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu wasiopungua 93,000 wamekwishapoteza maisha kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, ambavyo vilianza kama vuguvugu la kutaka mabadiliko.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com