1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas vyapamba moto

Amina Mjahid
12 Aprili 2024

Vikosi vya Israel vimepambana na wanamgambo wa Hamas kaskazini na katikati mwa Ukanda wa Gaza huku Israel ikisema imemuua kamanda wa kundi hilo aliyekuwa akipanga mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ya kiutu.

https://p.dw.com/p/4ehr2
 Khan Yunis
Mapambano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas yapamba moto Picha: Gil Cohen Magen/Xinhua News Agency/picture alliance

Wakaazi wa kambi ya wakimbizi ya Al - Nusseirat iliyopo katikati mwa Gaza wamesema watu kadhaa wameuawa au kujeruhiwa baada ya Israel kufanya mashambulizi kutokea angani, ardhini na baharini na kwamba misikiti miwili imeharibiwa. 

Kwa upande wake Israel imesema operesheni yake imefanikisha kuuawa kwa Ridwan Mohammed Abdullah, aliyeamuru kushambuliwa kwa msafara uliobeba misaada kwenye kijiji cha Jabalia kaskazini mwa Gaza kwa dhamira ya kundi la Hamas kupora shehena hiyo.

Haniyeh: Vifo vya wannagu Israel inajidanganya

Katika muda wa saa 24 zilizopita mamlaka za afya za Gaza zinazosimamiwa na Hamas zimesema mapigano yamesababisha vifo vya 89 ikiwemo 25 waliuawa na shambulizi la kombora lililoilenga nyumba katika kitongoji cha Al-Daraj.