Maoni: Je, Merkel atafanikiwa Afrika? | Matukio ya Afrika | DW | 12.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

ZIARA YA MERKEL AFRIKA

Maoni: Je, Merkel atafanikiwa Afrika?

Kansela Angela Merkel amekamilisha ziara yake barani Afrika iliyolenga kusaka mkakati wa pamoja wa kuwadhibiti wahamiaji wanaotoka Afrika kukimbilia Ulaya, lakini Ludger Schadomsky anasema hiyo si kazi rahisi.

Alipokuwa mjini Addis Ababa asubuhi ya Jumanne (11 Oktoba) uso wa Kansela Merkel haukonekana kuwa na furaha hata chembe mbele ya waandishi wa habari, baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu Hailemarian Desalegn.

Tangu awali, msemaji wake alishasema kwamba kiongozi huyo wa Ujerumani angelizungumzia masuala ya demokrasia na haki za binaadamu awapo Ethiopia. Na akatimiza ahadi yake.

Ukweli kwamba alipata ufasaha wa kuyazungumza hayo kinagaubaga kwenye ardhi ya mshirika huyo muhimu wa Ujerumani katika Pembe ya Afrika ni jambo la kusifiwa.

Kwa siku tatu, Kansela Merkel alikuwa ziarani katika mataifa matatu ya Afrika - Mali, Niger na Ethiopia - akiwa na ujumbe mkubwa mno kiasi cha kuisahaulisha kabisa ziara ya Waziri wake wa Mambo ya Nje, Frank-Walter Steinmeier, nchini Nigeria.

Schadomsky Ludger Kommentarbild App

Mkuu wa Idhaa ya Kiamhara ya DW, Ludger Schadomsky

Ikiwa ujumbe wa Ujerumani haukuwa umetosheka baada ya kupitia Mali na Niger, basi Waethiopia wangelikuwa na fursa ya kuifanya ziara hiyo fupi ikumbane na hisia kwamba yumkini Waafrika wanaweza wakawa washirika wazuri kwenye vita dhidi ya ugaidi na uhamiaji haramu, kuliko walivyo Waturuki, bali ikasadifu kuwa kuwasili wa Kansela Merkel kuliendana na muendelezo wa kuzimwa kwa mawasiliano ya intaneti, hapana shaka makaribisho yasiyopendeza kwa mshirika ambaye amekuwa akichangia mamilioni ya euro kwa miongo kadhaa sasa.

Ushirika usio uwiano

Jumla ya yote hayo, hapana shaka, ndiyo yaliyoakisika kwenye wajihi wa Kansela Merkel wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari. Upande mmoja anauhitaji utawala wa kikandamizaji wa Ethiopia, kwani unawahifadhi wakimbizi 800,000 wa Somalia, Sudan na Eritrea, kama vile Uturuki ilivyowachukuwa wakimbizi milioni 2.5 wa Syria. 

Kwa mtazamo wa kiorodha wa Berlin, bado Ethiopia ni kituo cha usalama, licha ya kwamba mamia ya watu wameuawa kwenye maandamano ya kuipinga serikali katika miezi ya hivi karibuni.

Endapo Ujerumani itashinikiza makubwa zaidi kwa serikali ya Ethiopia, basi utawala wa huko utawaachia wakimbizi waliomo kwenye ardhi yake wakasake mustakabali wao barani Ulaya.

Lakini pia haiwezi kufunga mikono yake wakati watu milioni 30 ya jamii ya Oromo wakikandamizwa na serikali yao na, hivyo, kulazimishwa kuwa wakimbizi wa siku zijazo.

Uwezekano wa mafanikio

Lakini je, haja anayoitafuta Kansela Merkel barani Afrika – yaani ushirika wa kuwazuia wakimbizi kumiminika barani Ulaya – inaweza kupatikana?

Moja ya jawabu ni kwamba hakuna suluhisho la haraka kiasi hicho kwa mataifa 54 ya bara hilo. “Ushirika huu wa Uhamiaji” hauwezi kufanya kazi.

Wajerumani na washirika wao barani Afrika wana mawazo yanayotafautiana kabisa kwenye hili. 
Akiwa mjini Addis Ababa, Kansela Merkel alisema hapo jana kwamba "ni jambo la muhimu kwa Afrika kutokuwapoteza raia wake wenye uwezo mkubwa wa kiakili."

Lakini uhalisia wenyewe huo. Hivi leo madereva wazuri wa teksi kwenye jiji la Washington, kwa mfano, ni Waethiopia wasomi, kwa sababu kwao hakuwaweki, hakuwapi matumaini ya kuishi vyema na watoto wao. 

Hata kama serikali ya Ujerumani inasema imejitolea kuanzisha programu za kuunda ajira mpya barani Afrika, lakini kama kazi zenyewe hazipo, usafirishaji binaadamu kwa magendo unageuka kuwa ajira inayowavutia vijana wengi barani humo.

Kwa vyovyote vile, ziara hii ya siku tatu imetupa mafunzo muhimu: Kwamba ikiwa Ujerumani na Ulaya zinataka kuisaidia kweli Afrika, basi kunapaswa kuwapo mpango madhubuti, kama ule uitwao "Marshall Plan."

Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com