1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maombi maalum dhidi ya janga la Corona yafanyika Tanzania

22 Aprili 2020

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kaasim Majaliwa ameiwakilisha serikali katika maombi maalum yaliofanywa na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kuliombea taifa dhidi ya janga la corona.

https://p.dw.com/p/3bFaS
Tansania Dar es Salaam | Kassim Majaliwa
Picha: Tanzania Presidents Office

Tanzania imekuwa taifa la tatu kufanya maombi haya ikitanguliwa na Kenya na Uganda. Viongozi wa dini katika madhehebu mbalimbali wamekutana pamoja katika viwanja vyenye historia ndefu ya nchi vya Karemjee jijini Dar es Salaam na kufanya ibada ya kitaifa kwa ajili ya kumuomba manani kulilinda taifa na janga la kidunia la virusi vya corona.

Maombi hayo yalioongozwa na waziri Mkuu Kaasim Majaliwa, yalizingatia taratibu zote za kiafya, ambapo kila aliyefika katika viwanja hivyo alifunika kinywa na pua kwa barakoa, umbali usiopungua mita moja kati ya mtu na mtu ulizingatiwa ili kudhibiti uwezekano wa maambukizi miongoni mwa wahudhuriaji.

Awali akifungua maombi hayo waziri Mkuu Majaliwa alielezea mikakati kadhaa ya serikali ambayo inaendelea kuchukuliwa ili kudhibiti kiwango cha maambukizi ambacho kinashuhudiwa kupanda siku hadi siku tangu taifa hilo lithibitishe kisa cha kwanza mnamo mwezi machi.

Wahudumu wajumuishwa kwenye sala ya kitaifa 

Tansania Dar es Salaam | Tansania Dar es Salaam | Gebet gegen Coronavirus
Picha: Tanzania Presidents Office

Katika maombi hayo ambapo takriban viongozi wa madhehebu ya kidini sita walihudhuria, ambapo wengi walinukuu vifungu na aya katika vitabu vitakatifu ikiwemo Quran tukufu pamoja na bibilia takatifu, wote wakionesha mwenyezi Mungu ndio kimbilio katika nyakati hizi ngumu ambazo taifa linapitia na dunia inapitia.

Katika maombi hayo ambayo wananchi walifuatilia kwa njia ya televisheni na radio viongozi wa dini pia waliwaweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu wahudumu wa afya, wagonjwa, walio chini ya ufuatiliwaji na wale waliopoteza maisha kwa ugonjwa huu hatari uliogharimu maisha ya zaidi ya watu milioni moja ulimwenguni kote huku ukihatarisha uchumi wa dunia.

Kufanyika kwa ibada hii ni matokeo ya mkutano uliofanyika Aprili tisa kati ya wizara ya afya na viongozi wa dini nchini, ambapo viongozi hao wa dini waliiomba wizara ya afya wafanye maombi kwa ajili ya taifa.

Chanzo: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam