Mandela yuko na familia yake leo Ijumaa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 18.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mandela yuko na familia yake leo Ijumaa

Lakini hajutii uamuzi wake

default

Mzee Mandela akiwa na wajukuu wake kuadhimisha miaka 90 ya kuzaliwa kwake

Leo Ijumaa Juni 18 mwaka wa 2008 ndio siku ya kuzaliwa kwa kiongozi mashuhuri wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela miaka 90 iliopita.Akiwa anasherehekea siku hii kijijini kwake,ametoa mwito watu maskini wasaidiwe.

Mzee Nelson Mandela, alizaliwa tarehe kama ya leo na mwezi huu huu,lakini mwaka wa 1918.

Kijiji chake alikozaliwa ni karibu na Qunu katika eneo la Transkei ya wakati huo, ambayo sasa inajulikana kama Cape ya Mashariki.

Babake alikuwa diwani wa Chief wa kabila lake la Thembu.Mbali na kuitwa Nelson Mandela lakini pia Roli-hla-hla nalo ni mojawapo wa majina yake.

Sasa ni maarufu kwa jina la Madiba.

Mzee Madiba, ambae anachukuliwa kama shujaa wa vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,pia aliingia katika daftari za historia kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa taifa hilo mweusi.Hilo lilitokea mwaka wa 1994, miaka minne baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani alikokuwa akitumikia kifungo cha maisha.

Lakini wakati wa kuachiliwa huru alikuwa ametimiza miaka 27 ndani, kwa kosa la uhaini.

Risala mbalimbali za pongezi kutoka kila pembe ya dunia zinazidi kumiminika,mkiwemo za Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,zikimtakia maisha marefu.

Mzee Madiba siku ya leo amekuwa kijijini kwake akiwa na familia yake ambayo aliikosa kwa kipindi cha miaka 27 akiwa ndani.

Alikuwa na watoto pamoja na wajukuu wake. Mwandishi habari mmoja amemuuliza ikiwa alitaka kuwa na familia yake wakati ule. Amejibu kuwa, yeye kama watu wengine walivyo angetaka hivyo.

Hata hivyo akaongeza kuwa hajutii hatua yake ya kukosa familia yake kwa mda mrefu.

Sherehe za kuzaliwa kwake za mwaka huu zimekwenda sambamba na zile za kuwa ndoa yake na mke wake wa sasa ambe ndie wa tatu imefikisha miaka 10.

Mkewe ni bi Graca Machel, mjane wa rais wa Msumbiji Samora Machel.

Walioana July 18 mwaka wa 1998.

Mkewe wa kwanza alikuwa Evelyn ambae alioana nae mwaka wa 1944 kabla ya kuachana mwaka wa 1957.

Leo Ijumaa Mzee Madiba, akiwa kwake Qunu akindamana na mkewe Graca, amesikitikia hali ya watu waliowengi ambao ni maskini nchini mwake.Amenukuliwa kusema kuwa umaskini umetanda nchini humo na kuongeza kuwa ukiwa maskini huwezi kuishi maisha marefu.

Amesema kuwa kuna watu wengi tajiri nchini humo ambao wanaweza kuchangia walichojaliwa na wenzao ambao hawana.

Bw Mandela alipochaguliwa kuongoza nchi hiyo aliahidi maisha mazuri kwa wote.Hata hivyo nyayo zake zimekuwa ngumu kufuata tangu ang'atuke baada ya kuwa madarakani kwa muhula mmoja tu.

Siku yake ya kuzaliwa imekuwa inatumiwa sana na wachambuzi kama kigezo kwa mrithi wake Thabo Mbeki.

Ingawa Afrika Kusini imekuwa ikiendelea kiuchumi lakini kiwango cha watu wasio na ajira kimebaki palepale kuwa asili mia 40 na uchunguzi unaonyesha kuwa pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kuongezeka .

 • Tarehe 18.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EetB
 • Tarehe 18.07.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EetB
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com