Mandela kuenziwa katika ibada kubwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mandela kuenziwa katika ibada kubwa

Dunia inaendelea kuomboleza kifo cha mzee Nelson Mandela. Jana rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alitangaza siku 10 za maombolezo kwa Mandela aliyefariki Alhamis usiku akiwa na umri wa miaka 95.

Maelfu ya watu wameweka maua kuonyesha mapenzi yao kwa Mandela

Maelfu ya watu wameweka maua kuonyesha mapenzi yao kwa Mandela

Ikulu ya Marekani imesema kuwa rais Barack Obama na mkewe Machelle watakwenda Afrika Kusini wiki ijayo kuungana na viongozi wengine wengi wa dunia, katika ibada ya kumuaga Nelson Mandela. Obama ambaye mwenyewe ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani, ataambatana na watangulizi wake wawili, George W Bush na Bill Clinton, ambao pia watasindikizwa na wake zao.

Rais Obama ataongoza ujumbe wa Marekani kwenye ibada ya kumkumbuka Mandela

Rais Obama ataongoza ujumbe wa Marekani kwenye ibada ya kumkumbuka Mandela

Mwili wa Mandela utawekwa katika jengo la serikali kwa muda wa siku tatu, kutoa fursa kwa wananchi wa Afrika Kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi waliyempenda. Baadaye mwili wake utasafirishwa kwenda kuzikwa mahali alipokulia Mandela, Qunu.

Ibada ya kumkumbuka Mandela

Jana maelfu ya raia wa Afrika kusini kutoka matabaka yote na rika zote walishiriki katika ibada ya pamoja ya dini mbali mbali, ambayo ilifanyika mjini Cape Town mahali ambapo Mandela alitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kuachiwa huru kutoka jela.

Mayor wa jiji la Cape Town Patricia de Lille alisema katika ibada hiyo kuwa watu wa mji huo, weusi kwa weupe, wahidi na wenye damu mchanganyiko, wanaungana kwa mshikamano kumuenzi Nelson Mandela na kukumbuka mchango wake kwa nchi yao.

Watu wa matabaka yote wamesononeshwa na kifo cha kipenzi wa dunia Nelson Mandela

Watu wa matabaka yote wamesononeshwa na kifo cha kipenzi wa dunia Nelson Mandela

Askofu mkuu wa zamani wa kanisa la Angikani nchini Afrika Kusini Desmond Tutu ambaye kama Mandela naye ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Amani, akijipangusa machozi ya huzuni alimsifu Mandela na kusema alikuwa alama ya umoja tangu alipoachiwa huru kutoka gerezani.

Kifo cha Mandela chaiunganisha dunia

Nchi kadhaa ulimwenguni zilitangaza maombolezo kwa kifo cha Nelson Mandela. Bendera zilipeperushwa nusu mlingoti katika baadhi ya nchi hizo, zikiwemo za kiafrika, Marekani, Ufaransa na Uingereza, na kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

India ilitangaza siku tano za maombolezo, na mnara maarufu wa mjini Paris, Eiffel, ulimeremeta kwa rangi za bendera ya Afrika Kusini kwa heshima ya Madiba.

Pande zenye misimamo tofauti kihistoria zimezungumza kwa sauti moja kumsifu Mandela; Wapalestina na Israel, Dalai Lama na China, Marekani na Iran wote wamemsifu kuwa mtu aliyetetea haki na usawa.

Ibada ya kumuaga Nelson Mandela ambayo itafanyika Jumanne ijayo kwenye uwanja wa mpira mjini Johannesburg inatarajiwa kuwa mojawapo ya mikusanyiko mkubwa ya watu maarufu kuwahi kutokea.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri:Amina Abubakar

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com