1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali: Raia washiriki kwenye duru ya pili ya kumchagua rais

12 Agosti 2018

Uchaguzi umefanyika chini ya ulinzi mkali na matokeo yanatarajiwa katika siku tano zijazo. Je rais Ibrahim Boubacar Keita anayemaliza muhula wake ataendelea kuliongoza taifa hilo linalokabiliwa na machafuko?

https://p.dw.com/p/332Ec
Mali Bamako - Wahl: Stichwahl des Präsidenten
Picha: Reuters/L. Gnago

Raia wa Mali Jumapili tarehe 12 mwezi huu wa Agosti wamepiga kura ya marudio katika uchaguzi wa rais. Kinyang'anyiro hicho ni kati ya Ibrahim Boubacar Keita aliyeko madarakani na kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse. Rais keita anatatetea muhula wa pili wa miaka mitano wa kuiongoza Mali.

Uchaguzi wa Jumapili ulianza kwa mvua nyepesi huku kukiwa na wapiga kura wachache waliojitokeza kwenye vituo vya kupigia kura. Watu wengi wana wasiwasi kuwa uchaguzi katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika unaweza kuvurugika kutokana na matatizo ya kiusalama. Katika uchaguzi wa kwanza wa rais uliofanyika mnamo tarehe 29 mwezi Julai wafanyakazi waliosimamia zoezi la kupiga kura waliuawa na vifaa vya kupigia kura viliharibiwa na makundi ya watu wenye msimamo mkali.

Vikosi vya usalama vya Mali vimesema vilizuia njama ya mashambulizi katika mji mkuu Bamako mnamo Jumamosi siku ya mkesha kabla ya kufanyika duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa rais. ambao uligubikwa na ukosefu wa usalama.Duru ya pili ya uchaguzi wa Jumapili huenda ikamrejesha madarakani Ibrahim Boubacar Keita licha ya kukosolewa vikali kwa namna anavyoongoza vita vya nchi hiyo dhidi ya wapiganaji wa jihadi na mashambulizi ya kikabila. Duru ya kwanza iliyoandaliwa mwezi uliopita, ilikumbwa na machafuko na vitisho kutoka kwa makundi yenye silaha ambayo yalisababisha kufungwa kwa mamia ya vituo vya kupigia kura na hasa katika eneo la kati ambalo linakabiliwa na machafuko.

Rais wa Mali anayetetea muhula wa pili  Ibrahim Boubacar Keita
Rais wa Mali anayetetea muhula wa pili Ibrahim Boubacar KeitaPicha: Reuters/A. Sotunde

Kufaulu kupata muhula wa pili wa kuongoza kwa rais Keita mwenye umri wa miaka 73 ni jambo ambalo linaonekana kuwa na uwezekano. kwenye duru ya kwanza kiongozi huyo alipata asilimia 41.7. Kiongozi huyo pia aliungwa mkono katika duru ya kwanza na mgombea aliyechukua nafasi ya tano pamoja na wagombea wengine ambao wanatoka katika eneo lake la kusini.

Kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse mwenye umri wa miaka 68, alipata asilimia 17.7 na hakuungwa mkono na mgombea yeyote katika duru ya kwanza, lakini anaungwa mkono na kiongozi maarufu wa kidini Mohamed Ould Bouye Haidara.

Ibrahim Boubacar Keita anatarajiwa kumshinda mpinzani wake kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse, licha ya kuongezeka kwa mapigano ya kikabila na mashambulizi ya makundi ya watu wenye msimamo mkali wakati wa utawala wake.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Mali ilikumbwa na machafuko ishara kwamba makundi ya wapiganaji, baadhi yaliyoungana na makundi ya kigaidi ya al Qaeda na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS yamejikusanya upya tangu Ufaransa ilipoyapeleka majeshi yake nchini Mali mnamo mwaka 2013.

Soumaïla Cissé, kiongozi wa upinzani anayegombea urais kwenye uchaguzi wa 2018 nchini Mali
Soumaïla Cissé, kiongozi wa upinzani anayegombea urais kwenye uchaguzi wa 2018 nchini Mali Picha: DW/K. Gänsler

Sasa ushawishi wa makundi hayo unazidi kukua katika katika eneo la jangwa la kaskazini mwa Mali na pia katika maeneo mengine ya kati. Uwepo wao katika taifa hilo kubwa la Afrika Magharibi pamoja na uwezo wao wa kueneza vurugu hadi katika majirani zake kumezifanya nchi za Magharibi kuipa Mali kipaumbele na kuiweka juu katika orodha yake ya masuala ya usalama. Mtawala wa kikoloni wa zamani, Ufaransa na mshirika wake Marekani wamepeleka maelfu ya askari katika kanda hiyo.

Mapigano ya kikabila na mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi vimesababisha mivutano zaidi na kutokuaminiana katika nchi hiyo. Kiongozi wa upinzani anamlaumu rais Keita kwa ukosefu mkubwa wa usalama, machafuko na rushwa nchini Mali. Chama chake cha upinzani pia kimesema kulikuwa na udanganyifu wa kura katika uchaguzi wa mwezi Julai.

Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki na matokeo yanatarajiwa kutangazwa katika kipindim cha siku tano zijazo. msaidizi katika ofisi ya waziri mkuu amesema usalama umeimarishwa katika uchaguzi wa duru ya pili kwa asilimia 20 zaidi ya askari wanaojibika ulinda usalama.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/APE/RTRE

Mhariri: Bruce Amani