Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ziarani China | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ziarani China

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden amesema eneo la ulinzi katika anga ya China limesababisha wasiwasi mkubwa na China inahitaji kupunguza wasiwasi huo katika eneo la Bahari ya Mashariki mwa China ili kulinda amani.

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden akisalimiana na Rais wa China Xi Jinping

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden akisalimiana na Rais wa China Xi Jinping

Akizungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa Marekani kwenye mji mkuu wa China, Beijing, Biden ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatua ya China kuweka eneo jipya la ulinzi wa anga yake kwenye Bahari ya China Mashariki na amesema amelizungumzia suala hilo wakati wa mkutano wake na Rais Xi Jinping, yaliyodumu kwa saa nne. Biden ameyatoa matamshi hayo mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini China.

Biden amesema alimueleza Jinping kuhusu msimamo imara wa Marekani kufuatia hatua ya China kuweka eneo jipya la ulinzi mwezi uliopita katika eneo la visiwa vinavyozozaniwa kati yake na Japan na kusema kuwa ndege zote zitakazopita kwenye anga hiyo lazima ziiarifu nchi hiyo. Hatua hiyo iliikasirisha Marekani na kusababisha ipeleke ndege zake mbili za kijeshi aina ya B52 katika eneo hilo.

Joe Biden akizungumza na wafanyabiashara wa marekani huko China

Joe Biden akizungumza na wafanyabiashara wa marekani huko China

Hakuna yeyote kati ya Biden na Jinping aliyetoa tamko lolote kuhusiana na mvutano huo baada ya mazungumzo yao ya jana Jumatano. Hata hivyo, viongozi hao wawili walizungumzia maslahi ya kiusalama ya Marekani na China. Kwa upande wake China leo imeiambia Marekani kuwa hatua ya kuweka eneo la ulinzi inaambatana na sheria na mkataba wa kimataifa. Msemaji wa wizara hiyo, Hong Lei amesema wito huo umetolewa kwa Biden aliyekutana na Rais Jinping na Makamu wa Rais, Li Yuanchao na kuitaka Marekani ilichukulie suala hilo kwa haki.

Biden aikosoa China kuhusu uhuru wa habari

Ama kwa upande mwingine Biden leo ameikosa China jinsi inavyowadhibiti waandishi wa habari wa kigeni. Kauli hiyo ameitoa baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang na siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuzungumzia suala kama hilo wakati alipokutana na Rais Jinping. Biden amesema kuwa Marekani na China bado zina tofautiana katika mambo mengi, ikweimo jinsi China inavyowachukulia waandishi wa habari wa Marekani.

Biden amesema ubunifu mzuri unapatikana mahali ambapo watu wanapumua kwa uhuru, wanazungumza kwa uhuru, wana uwezo wa kukosoa na ambako magazeti yataripoti ukweli bila kuhofia madhara yake. Ameongeza kusema kuwa China inahitaji kuchukua hatua kadhaa kufungua njia yake ya kisiasa na kijamii pamoja na uchumi wake, lakini hakufafanua zaidi.

Joe Biden alipowasili nchini China,akikagua gwaride.

Joe Biden alipowasili nchini China,akikagua gwaride.

Biden ambaye aliwasili China siku ya Jumanne akitokea Japan, alikosolewa na magazeti ya China kwa kuegemea upande wa Japan na kufumbia macho uchokozi unaofanywa na nchi hiyo. Baadaye mchana wa leo Biden anatarajiwa kuelekea Korea Kusini, kituo cha mwisho cha ziara yake ya barani Asia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com