1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiSomalia

Maharamia Somalia waibuka upya wakilenga meli za biashara

11 Mei 2026

Wakati meli zikitafuta njia nyingine ya kufika Afrika ili kukwepa kanda ya Mashariki ya Kati iliyokumbwa na mzozo, maharamia wa Somalia wanatajwa kuibuka upya, hatua iliyosababisha ongezeko la gharama za bima.

https://p.dw.com/p/5DbcU
Somalia Konflikt
Picha: MOHAMED DAHIR/AFP/Getty Images

Kwa muda wa miezi miwili, usafirishaji duniani umekumbwa na jinamizi, wakati ambapo Mlango Bahari wa Hormuz ukiendelea kufungwa kwa kiasi kikubwa kwa meli za kibiashara na kitisho cha mashambulizi mapya ya meli katika Bahari ya Shamu.

Na sasa, mzozo wa tatu unanyemelea, nao ni kuibuka upya kwa maharamia wa Somalia. Hata kabla ya kuongezeka kwa uhasama baina ya Marekani, Israel na Iran, karibu nusu ya meli zote zilizokuwa zikielekea Ulaya, Asia na Ghuba ya Aden, zililazimika kupita Bahari ya Shamu na Mfereji wa Suez kutokana na mashambulizi ya awali ya Wahuthi wanaoungwa mkono na Iran.

Yakikabiliwa na kitisho cha mashambulizi katika mlango bahari wa Bab el-Mandeb, ujia mwembamba unaounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, makampuni makubwa badala yake yaliamua kuchagua njia ndefu ya kuzunguka kusini mwa Afrika.

Njia hiyo hata hivyo iliongeza muda wa safari kwa wiki mbili au tatu, yakizifanya meli kupita karibu na pwani ya Somalia, ambako miaka michache iliyopita maharamia waliendesha kampeni ya utekaji wa meli kwa miaka kadhaa iliyofikia kilele mwaka 2011. Tangu wakati huo, matukio ya hapa na pale yamekuwa yakiripotiwa.

Uharamia katika bahari ya Hindi
Maharamia wa Kisomalia wakiwa wamekamatwa 2024Picha: Indian Navy/AP/picture alliance

Kuzuka upya kwa Maharamia kunazidisha wasiwasi

Sehemu hiyo ya bahari sasa inashuhudia uharamia ukirejea kwa nguvu kubwa,  ambapo meli tatu zimetekwa nyara karibu na pwani ya Somalia na Yemen katika kipindi cha wiki tatu zilizopita pekee. Kufikia tarehe 8 Mei 2026, meli za mafuta za Honour 25 na Eureka pamoja na meli ya mizigo Sward bado ziko chini ya udhibiti wa maharamia.

Mtafiti mwandamizi wa masuala ya vitisho vya kimataifa na uhalifu uliopangwa katika Taasisi ya Masuala ya Usalama ya Afrika Kusini Tim Walker,  anasema maharamia sasa wanaona vizuizi vimepungua katika ukanda wa pwani wa Somalia wenye urefu wa kilomita 3,300 ambao ndio mrefu zaidi barani Afrika.

Aliieleza DW kuwa "baadhi ya makundi yanayoratibiwa na vinara wa uharamia, sasa yanaangalia kuteka meli na kuzishikilia kwa ajili ya fidia, pamoja na wafanyakazi waliomo ndani wakati mwingine wakidai fedha kubwa kama malipo ya kuwaachia salama.”

Maharamia walio na ufadhili hutumia mashua

Kulingana na kampuni ya takwimu za masuala ya baharini ya Lloyd's List Intelligence, kuna angalau makundi mawili ya maharamia yanayofanya kazi kwa sasa, hasa yakijikita Puntland, eneo lenye mamlaka ya kujitawala kiasi kaskazini-mashariki mwa Somalia.

Ripoti zinasema Maharamia wameteka vyombo vikubwa vya jadi vinavyojulikana kama dau, vinavyotumika kwa uvuvi na biashara za ndani na kuvitumia upya katika shughuli zake. Mbinu hiyo imewawezesha kupanua eneo lao la operesheni na kubaki baharini kwa wiki kadhaa kabla ya kuvitumia kama vituo vya kuanzia kushambulia meli za kibiashara.

Ubelgiji Zeebrugge 2010 | Jeshi la Wanamaji la Ubelgiji likiendesha zoezi la kupambana na uharamia 2010
Jeshi la Wanamaji la Ubelgiji likiendesha zoezi la kupambana na uharamia 2010Picha: Wang Xiaojun/Xinhua/IMAGO

Uharamia unaweza kuongeza zaidi gharama za usafirishaji

Wakati migogoro ya Mashariki ya Kati tayari ikiongeza gharama za bima za usafirishaji baharini, kufikia takribani dola milioni moja katika gharama za mafuta kwa kila safari na kusababisha viwango vya usafirishaji kupanda kwa kasi, viongozi wa sekta ya usafirishaji wanaonya kuwa kurejea kwa kiwango kikubwa kwa uharamia kunaweza kuongeza gharama hata zaidi na kuvuruga biashara ya kimataifa zaidi.

Katika mgogoro wa awali wa uharamia mwaka 2011, athari za kiuchumi zilizotokana na utekaji wa meli zilikadiriwa kufikia takribani dola bilioni 7 kwa mwaka, kulingana na taasisi ya utafiti ya Sasakawa Peace Foundation ya Japan.

Hiyo ilijumuisha gharama za operesheni za kijeshi, kubadilisha njia za safari, kusafiri kwa kasi zaidi ikimaanisja kutumia mafuta zaidi pamoja na vifaa vya ziada vya usalama na walinzi walioko ndani ya meli.

Fedha za maendeleo kwa Somalia zapunguzwa

Wakati vita vya Iran viliwapa maharamia fursa ya kujificha kwa muda, mabadiliko ya sera ya Washington kuelekea Afrika Mashariki huenda pia imechangia kurejea kwa uharamia.

Kwa miaka mingi, Marekani ilifadhili miradi ya maendeleo nchini Somaliahasa katika jamii za pwani ili kupunguza umaskini na kuwazuia vijana kujiunga na makundi ya uharamia.

Hata hivyo, chini ya utawala wa sasa wa Trump, karibu misaada yote ya maendeleo isiyohusiana na usalama imesitishwa. Badala yake, Washington imeelekeza nguvu kwenye operesheni za moja kwa moja za kupambana na ugaidi dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab.