Mahakama Pakistan yasitisha kifungo cha Khan na mkewe
1 Aprili 2024Khan amekuwa akikabiliwa na kesi zaidi ya 200 za kisheria tangu alipong'olewa madarakani Aprili 2022, katika kile alichokitaja kuwa ni kampeni ya kumuweka madarakani.
Khan, mwenye umri wa miaka 71, anasalia gerezani kuhusiana na kesi nyingine mbili ikiwemo ya uhaini na ndoa isiyo halali zikiwa na kifungo cha hadi muongo mmoja.
Soma pia: Imran Khan na mkewe washtakiwa kwa ufisadi
Msemaji wa chama chake cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) alisema Mahakama Kuu ya Islamabad ilitupilia mbali hukumu za wawili hao zilizotolewa na mahakama ya kupambana na ufisadi kuhusiana na kuuza zawadi za serikali, huku rufaa dhidi ya hukumu yao ikisubiriwa.
Mahakama ya usikilizaji kesi iliruhusu "mawakili wachache lakini pia ilikuwa imefikia uamuzi huo kwa haraka bila kuruhusu utetezi kuhitimisha hoja," msemaji Ahmed Janjua alisema.
Khan alikuwa tayari amefungwa jela na kuzuiwa kugombea wadhifa wa umma baada ya kuhukumiwa vifungo vitatu siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Februari 8 nchini Pakistan.
Soma pia: Wapinzani wa waziri mkuu wa zamani Pakistan Khan kuunda serikali ya muungano
Mke wake Bushra Bibi pia alihukumiwa kwa ufisadi na ndoa ambayo mahakama ilisema ilikuja haraka sana baada ya talaka yake, kinyume na sheria za Kiislamu.
Wachambuzi walisema zilikuwa jitihada za kukamilisha kutengwa kwa waziri mkuu huyo wa zamani na chama chake cha PTI kwenye uchaguzi huo ambao ulikumbwa na madai mengi ya wizi wa kura kabla na baada ya kura.
Khan asalia kuwa maarufu miongoni mwa wapigakura
Licha ya ukandamizaji wa kukamatwa na udhibiti, wagombea watiifu kwa Khan walipata viti vingi kuliko chama kingine chochote lakini walipungukiwa kwa mbali wingi unaohitajika kutawala.
Muungano wa vyama vyenye uhusiano wa karibu na taasisi yenye nguvu ya kijeshi ya Pakistan umechukua madaraka, ukiongozwa na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif.
Khan alisaidiwa kuingia madarakani kwa kuungwa mkono na viongozi wakuu wa jeshi mnamo 2018 lakini aliondolewa ofisini kwa kura ya kutokuwa na imani naye miaka minne baadaye baada ya kufarakana vibaya na jeshi.
Akiwa kiongozi wa upinzani aliendesha kampeni ya kukaidi jeshi, na kulituhumu kula njama na Marekani ili kumuondoa madarakani na kupanga njama ya kumuua ambamo alijeruhiwa kwa risasi.
Soma pia: Matokeo ya awali yawapa ushindi wafuasi wa Imran Khan
Wachambuzi wanasema jeshi -- ambalo limeitawala Pakistan moja kwa moja kwa miongo kadhaa ya historia yake na linaendelea kuwa na nguvu kubwa nyuma ya pazia - lilijaribu kumfungia nje ya siasa za kiraia ili kulipiza kisasi.
Wiki iliyopita, majaji sita waandamizi kutoka Mahakama Kuu ya Islamabad waliyashtumu mashirika ya kijasusi -- ambapo lenye nguvu zaidi kati yake linasimamiwa na jeshi -- kuwashurutisha kubadili hukumu zao kesi zikiwemo zinazomhusu Khan.
Serikali imeahidi kuchunguza malalamiko ya majaji hao, ambao wamedai walitishwa na kufuatiliwa na maafisa wa upelelezi.