Macron aiomba Ulaya kuikemea Uturuki | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Macron aiomba Ulaya kuikemea Uturuki

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameiomba Ulaya kuonyesha mshikamano wa pamoja katika kukemea hatua isiyokubalika ya Uturuki, wakati akijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mataifa ya eneo la Mediterania

Ufaransa kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiiuga mkono Ugiriki na Cyprus katika mzozo unaoongezeka na Uturuki kuhusu rasilimali na ushawishi wa jeshi la wana maji katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterania ulioibua wasiwasi wa kuzuka kwa mzozo mbaya zaidi. Soma zaidi: Ufaransa mwenyeji wa mkutano wa mataifa ya Mediterania

Mzozo huo tayari umechochea kuongezeka kwa wasiwasi kati ya Uturuki na Ulaya, na hasa kutokana na uingiliaji wa kijeshi wa Uturuki nchini Libya, sera yake kuelekea nchini Syria pamoja na hatua kali dhidi ya wapinzani wa Rais Recep Tayyip Erdogan. Macron aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano huo kwenye kisiwa cha Ufaransa cha Corsica kwamba Ulaya inatakiwa kuwa na msimamo kuelekea hatua hizo zisizokubalika.

Frankreich, Korsika I Präsident Emmanuel Macron

Macron yuko ziarani Corsica

Alisema, kwa sasa Uturuki sio tena mshirika katika ukanda wa mashariki mwa Bahari ya Mediterania kutokana na hatua zake hizo, ingawa anatarajia kuanzisha mazungumzo na taifa hilo. Muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Macron, Uturuki ilitoa tamko lake la kuyalaani na kuyaita kuwa ni ya kiburi. Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki imesema Macron kwa mara nyingine ametoa matamshi yaliyojaa jeuri na yalikuwa ni ishara tosha ya udhaifu wake na kukata tamaa. Soma zaidi: Erdogan anasema Uturuki itasimama kidete kutetea haki zake

Katika mjadala kuhusiana na namna Erdogan anavyoushughulikia mzozo huo ambao Ugiriki inataka Uturuki iadhibiwe kwa vikwazo vikali vya kiuchumi, Macron alisema watu wa Uturuki walio wazuri wanastahili kitu bora zaidi.

Wizara hiyo ya mambo ya kigeni ya Uturuki imemtuhumu Macron, aliyeyaunga mkono madai ya Ugiriki kwa kupeleka manowari za kivita za Ufaransa kwenye eneo linalozozaniwa ikisema alipeleka vikosi hivyo kwa mtizamo wake binafsi na wa kitaifa, na kuongeza kuwa hatua za Macron zinaiweka Ulaya na maslahi mapana ya Umoja wa Ulaya katika hatari kubwa. Mkutano huo wa kilele unawakutanisha viongozi wa Ufaransa, Italia, Malta, Ureno, Uhispania, Ugiriki na Cyprus.