1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

Maandamano yaendelea Ufaransa kupinga mageuzi ya pensheni

23 Machi 2023

Vyama vya wafanyakazi nchini Ufaransa vimesalia katika msimamo wao wa kupinga mageuzi ya mfumo wa pensheni unaopigiwa upatu na Rais Emmanuel Macron ambaye ameahidi kuwa mpango huo utatekelezwa mwishoni mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4P73F
Themenpaket | Streik und Proteste in Frankreich
Picha: ERIC GAILLARD/REUTERS

Maandamano hayo ambayo yalianza katikati mwa mwezi Januari tayari yameanza kushuhudiwa hii leo katika usafiri wa treni. Shirika la reli la kitaifa SNCF limesema kuwa nusu ya safari zote za treni za mwendo kasi zilifutwa  baada ya vyama vya wafanyakazi kubaini kuwa karibu theluthi moja ya wafanyikazi wangefanya mgomo. Angalau nusu ya idadi za treni kuelekea mji mkuu Paris kutoka vitongoji mbalimbali hazikufanya kazi leo Alhamisi.

Katika kitongoji cha Nanterre, Paul Kantola, fundi seremala mwenye umri wa miaka 57, anasema amelazimika kuamka saa kumi na moja alfajiri ili aweze kupata usafiri wa kuelekea kazini, lakini amesisitiza kuwaunga mkono waandamanaji, na kusema kwamba inatisha kuzeeka katika mazingira kama hayo, wakati tayari unapokuwa umestaafu, mapato yako yanakuwa  hayakutoshelezi.

Rais Macron mwenye umri wa miaka 45 hapo jana alisema kuwa yuko tayari kuona umaarufu wake na kukubalika vinapungua miongoni mwa Wafaransa kwa sababu mswada wa kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64 ni muhimu na kwa maslahi jumla ya nchi hiyo.

Akifanya kazi kwa maagizo ya Macron,  Waziri Mkuu Elisabeth Borne  alipendekeza wiki iliyopita kifungu katika katiba  cha kuweza kupitisha mageuzi bila kura ya Bunge. Siku ya Jumatatu, Serikali ilinusurika na kura ya kutokuwa na imani nayo, lakini hali hiyo imezua mzozo mkubwa wa ndani katika muhula wa pili wa Macron.

Mpango wa mageuzi wa pensheni waathiri umaarufu wa Macron

Themenpaket | Streik und Proteste in Frankreich
Kikaragosi kinachomuonyesha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati wa maandamano ya kitaifa ya kupinga mageuzi ya pensheni huko Nice, Ufaransa, Machi 23, 2023.Picha: ERIC GAILLARD/REUTERS

Uchunguzi wa Jumapili ulionyesha kuwa Macron anakubalika kwa asilimia 28 tu miongoni mwa wafaransa, ikiwa ni kiwango chake cha chini zaidi tangu kushuhudiwe lile vuguvugu la "vizibao vya njano" la kuipinga serikali maarufu kama "Gilets Jaunes" mnamo mwaka 2018-2019.

Maandamano yamekuwa yakishuhudiwa nchini Ufaransa katika siku za hivi karibuni, na kusababisha mamia ya watu kukamatwa huku Polisi wakishutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuenea kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi na kukamatwa kiholela kunakoripotiwa katika vyombo kadhaa vya habari.

Soma pia: Macron ashikilia mageuzi ya pensheni kufanyika Ufaransa

Siku ya Jumatano jioni, mamia ya watu waliandamana tena katika mji mkuu Paris, mji wa kusini-mashariki wa Lyon na mji wa kaskazini wa Lille, ambako watu wawili walikamatwa kwa tuhuma kuharibu mali ya umma.

Wakusanyaji taka wa manispaa ya Paris wameahidi kuendelea na mgomo hadi Jumatatu, huku maelfu ya tani za taka zikitapakaa mitaani, na kuharibu mandhari ya jiji hilo maarufu. Vizuizi katika viwanda vya kusafisha mafuta vitaendelea pia na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa mafuta nchini Ufaransa.

(AFPE)