1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yaharibu silaha zake za kemikali

Mjahida5 Februari 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Libya Mohamed Abdelaziz amesema nchi hiyo imeharibu kabisa silaha zake za kemikali zilizopatikana chini ya uongozi wa rais wa zamani Moamer Qadhafi.

https://p.dw.com/p/1B2yK
Wataalamu wa OPCW
Wataalamu wa OPCWPicha: Philipp Guelland/AFP/Getty Images

"Libya imekuwa nchi huru kabisa kutotumia silaha za kemikali zilizotoa kitisho kwa usalama wa jamii,mazingira na nchi jirani," Alisema Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Libya Mohamed Abdelaziz.

Waziri huyo amesema hatua iliyopigwa na nchi hiyo isingewezekana bila ya uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa ikiwemo Canada na Marekani kwa kutoa usaidizi wa kiteknologia na kiufundi katika kutokomeza silaha hizo.

Abdelaziz alitangaza haya katika mkutano na waandishi habari uliohudhuriwa na mkuu wa shirika la udhibiti wa silaha za kemikali (OPCW) Ahmet Uzumcu aliyosema juhudi za kimataifa zilizofanikisha hilo nchini Libya sasa zinaangaliwa jinsi zitakavyofanikisha zoezi la Syria la kuharibu silaha zake.

Hata hivyo shirika hilo lililo na makaazi yake mjini The Hague Uholanzi limethibitisha uharibifu wa kemikali za Libya na kusema, uharibifu huo wa mabomu na gesi ya sumu ulifanyika january 26.

Mkuu wa shirika la OPCW Ahmet Üzümcü
Mkuu wa shirika la OPCW Ahmet ÜzümcüPicha: Reuters

Uzumcu pamoja na wataalamu kutoka Marekani Ujerumani na Canada tayari wameshafanya ziara ya kuthibitisha hilo katika eneo la Ruwagha mahali kulipoharibiwa silaha hizo za kemikali.

Libya yaharibu silaha zake baada ya miaka takriban tisa

Aidha hatua ya kuanza kuharibu silaha za kemikali nchini Libya zilianza mwaka wa 2004 wakati Libya ilipojiunga na muungano wa kudhibiti silaha za kemikali ambapo wanachama wanapaswa kuharibu silaha zote walizonazo nchini mwao.

Huku hayo yakiarifiwa Oparesheni ya kuangamiza silaha za Syria iliyoridhiwa na serikali ya nchi hiyo mwaka uliopita baada ya shinikizo la Marekani iliyotishia kuingilia kijeshi nchi hiyo endapo haitoharibu silaha zake inasemekana kuendelea kwa kasi ndogo hatua ambayo imezua wasiwasi mkubwa kwa Marekani.

Ramani ya Libya
Ramani ya Libya

Syria imethibitisha kuwa na tani 7000 za silaha hizo hatari ambazo zilitarajiwa kuhamishwa kutoka nchini humo kabla ya Disemba tarehe 31 mwaka uliopita.

Hapo jana Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa Syria ilisema nchi hiyo itaanza kuhamisha silaha zake mwezi huu wa February huku wapinzani wakiitaka nchi hiyo kuushawishi utawala wa Syria kuzingatia suala la kuwepo kwa serikali ya mpito Syria, nchi inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Gennady Gatilov ameliambia shirika la habari nchini humo kwamba, nchi hiyo iko tayari kutekeleza zoezi hilo ifikapo tarehe mosi mwezi wa Machi chini ya makubaliano ya shirika la OPCW.

Mkuu wa Upinzani Syria Ahmad Jarba na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov
Mkuu wa Upinzani Syria Ahmad Jarba na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters

Amesema Syria imepanga kuhamisha kiwango kikubwa cha kemikali hiyo mwezi huu.

Gatilov amesema Syria imechelewa kuhamisha silaha zake za kemikali kutokana na masuala ya usalama lakini ina nia ya kufanya hivyo kabla muda wa misho kufikiwa.

Tamko hili limekuja wakati mkuu wa upinzani Syria Ahmad Jarbaa akikutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov katika jitihada za kuushawishi utawala wa Bashar al Assad uzingatie hatua ya kuundwa kwa serikali ya mpito.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri Yusuf Saumu