1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu atakiwa kuzingatia mpango wa kusitisha vita Gaza

1 Juni 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Israel Yair Lapid amemtolea mwito Waziri Mkuu wa taifa hilo Benjamin Netanyahu, kuzingatia mpango uliotangazwa na rais wa Marekani Joe Biden wa kusitisha mapigano Gaza

https://p.dw.com/p/4gWy0
Israel Jair Lapid
Kiongozi wa upinzani Israel amtaka Netanyahu kuzingatia mpango wa kusitisha mapigano Gaza Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Lapid pia ametoa pendekezo la kuiunga mkono serikali iwapo  washirika wa serikali ya Netanyahu wataukataa mpango huo uliotangazwa na Biden. 

Familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas wametaka pande zote mbili kuukubali mpango huo wa kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi minane sasa na kutaka jamaa zao kurejea nyumbani, lakini Israel imeendelea kusema masharti ya kusitisha mapigano lazima yatimizwe kwanza. 

Biden hapo jana alielezea namna mpango huo wa hatua tatu wa kusitisha mapigano utakavyotekelezwa.

Wizara ya afya ya Gaza yasema karibu watu 36,000 wameuawa Gaza

Hatua ya kwanza itakuwa ni kipindi cha wiki sita cha usitishaji mapigano ambacho kitashuhudia vikosi vya Israel vikiondoka kwenye miji yote iliyo na watu wengi kwenye Ukanda wa Gaza.

Kisha itafuatiwa hatua ya pili na ya tatu inayojumuisha kubadilishana mateka wote na wafungwa, na baadae vikosi vya Israel vitaondoka kikamilifu na mpango wa kuijenga upya Gaza utaanza.