Kinyang′anyiro cha kuania madaraka ya ANC Afrika Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 05.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kinyang'anyiro cha kuania madaraka ya ANC Afrika Kusini

Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini yu kifua mbele katika kinyang'anyiro cha kudhibiti madaraka dhidi ya wapinzani wake ndani ya chama tawala cha ANC,mkutano mkuu wa chama hicho utakapoitishwa December mwaka huu.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Kimsingi atakaechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha ANC mwezi December, atakabidhiwa wadhifa au ataendelea kuwa rais,uchaguzi utakapoitishwa mwaka 2014 ila kama kutakuwa na makubaliano fulani yatakayofikiwa,kama vile vyombo vya habari vinavyoashiria nchini humo.

Hadi wakati huu,mtu pekee aliyejitokeza kuania wadhifa wa mwenyekiti wa chama hicho,mkutano mkuu utakapoitishwa huko Mangaung kuanzia December 16 hadi 20,rais Jacob Zuma,anaweza kutegemea uungaji mkono wa wajumbe wa jimbo la Kwazulu-Natal,mahala alikozaliwa ambalo pia ni ngome yake ya kisiasa.

Idadi ya wawakilishi wa kabila la Zulu imeongezeka kwa ghafla na kufikia asili mia 36-hali inayotokana na kuongezeka idadi ya wanaoomba uwanachama na pia utaratibu wa kugawa majimbo uliokubaliwa kwa siri na wakuu wa chama hicho.

Kwa namna hiyo rais Jacob Zuma anaweza kutegemea uungaji mkono madhubuti wa wajumbe 974 toka jumla ya wajumbe 4500 watakaokutana kuwachagua viongozi wepya watakaokiongoza chama cha ANC katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

ANC Anhänger in Pretoria

Wafuasi wa ANC mjini Pretoria

Jengine linaloweza kumfurahisha rais Zuma ni ile hali kwamba katika wakati ambapo wazulu wanapanga kumiminika kwa wingi mkutanoni,wenzao wa Mashariki ya Cap-eneo alikozaliwa Nelson Mandela ambalo ni ngome ya watu wa kabila la Xhosa,wanaonyesha kudhoofika.

Inasemekana wafuasi wamekipa kisogo chama cha ANC katika eneo hilo na baadhi ya makundi hayajakamilisha masharti ya kuweza kutuma mwakilishi katika mkutano mkuu ujao.Kundi la watu wa kabila la Xhosa ni la pili kwa ukubwa katika mkutano mkuu lakini litawakilishwa na wafuasi 676 tu.

"Kwa namna hiyo,Zuma anaweza kushinda kwa wingi mdogo tu" anahisi bibi Mari Harris-mkurugenzi wa taasisi ya uchunguzi wa maoni ya umma IPSOS Markinor."Lakini mambo yanaweza kubadilika".Ameongeza kusema kwa tahadhari.

Wadadisi hawajasahau funzo la mwaka 2007 pale mtangulizi wa Jacob Zuma,rais wa wakati ule Thabo Mbeki alipolazimika kujiuzulu kufuatia zilzala ya kisiasa ambayo hakuna aliyeitegemea.

Hakuna kinachoonyesha kwamba Zuma hatoweza kukumbana na mkasa kama huo katika wakati ambapo uongozi wa chama unazongwa na hila za kila aina kuanzia mifarakano hadi kufikia makubaliano ya kichini chini yanayochanganya kila kitu kuanzia nadharia za kisiasa,watu na hali mahsusi ya kimkoa na lugha.

Chama cha ANC kinachukua sura ya chama pekee katika nchi ambako licha ya malalamiko ya umma,wengi wa wananchi wanashindwa kukigeukia chama kilichoung'owa madarakani utawala wa ubaguzi wa rangi na mtengano-Apartheid.

Kuna baadhi wanaashiria mustakbal ambao si mzuri kwa ANC na kufika hadi ya kuzungumzia "mageuzi au maangamizi",kama alivyosema hivi karibuni mmojawapo wa viongozi wa chama,waziri wa makaazi Tokyo Sexwale.

Südafrika Präsident Jacob Zuma und seine drei Ehefrauen

Rais Jacob Zuma akizungukwa na wake zake wote watatu

Ikiwa kilichosemwa na gazeti la The Star,toleo la alkhamisi iliyopita,ni kweli,basi eti rais Zuma amempatia "tikiti "isiyokuwa na mfano makao wake wa rais Kgalema Motlanthe.

Eti wamekubaliana Zuma aendelee kuongoza chama cha ANC na kumuachia Montlanthe nafasi ya kupigania wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa mwaka 2014.

Mwanaharakati huyo wa zamani wa haki za wafanyakazi anajivunia umashuhuri mkubwa miongoni mwa wananchi:asili mia 51 wanamuunga mkono dhidi ya 48 wanaomuunga mkono Jacob Zuma.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef