1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta aongoza

5 Machi 2013

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa rais nchini Kenya, yanaonesha kuwa mgombea anayekabiliwa na mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) anaongoza hadi sasa, huku hali ikiendelea kuwa shwari.

https://p.dw.com/p/17qVD
Kenya's Deputy Prime Minister and Jubilee Alliance Presidential candidate in the upcoming Presidential elections, Uhuru Kenyatta, addresses surpporters during a plotical rally in the capital Nairobi on February 13, 2013. Kenya's eight presidential candidates held the country's first ever face-to-face debate this week as tensions mount ahead of next month's election, five years after bloody violence erupted in the wake of the last vote. While two main candidates -- Uhuru Kenyatta and Raila Odinga -- dominate the race for the March 4 election, all the hopefuls have potential influence, especially if voting goes to a second round run-off. AFP PHOTO / SIMON MAINA (Photo credit should read SIMON MAINA/AFP/Getty Images)
Kenia Wahlen Uhuru KenyattaPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Huku kiasi cha robo moja ya kura kikiwa kimeshahisabiwa, matokeo ya awali yanaonesha kuwa Kenyatta, ambaye pia ni naibu waziri mkuu, anaongoza kwa asilimia 54 ya kura, akifuatiwa na Waziri Mkuu Raila Odinga mwenye asilimia 41.

Hata hivyo, ni kura chache zilizokuwa zimehisabiwa kutoka kwenye ngome ya Odinga, mji wa Kisumu ulio magharibi mwa Kenya, na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema kwamba matokeo yatakamilika kufikia kesho Jumatano (tarehe 6 Machi).

Hapo jana Jumatatu (tarehe 4 Machi), wapiga kura walijitokeza kwa wingi kupiga kura. Maafisa wa IEBC wanakisia kwamba kiasi cha asilimia 70 ya raia milioni 14 waliojiandikisha, wamepiga kura zao.

Kwa upande mwengine, mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na makundi ya watu wanaotaka kujitenga kwenye eneo la pwani ya Kenya yaliua watu 19 hapo jana, huku mashambulizi mengine yakiripotiwa kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia, ingawa sehemu kubwa ya nchi ilipiga kura kwa amani.

Hali ni shwari

Hadi asubuhi ya leo Jumanne (tarehe 5 Machi), mji mkuu Nairobi ulikuwa kimya na hakukuwa na matukio mengine ya ghasia yaliyoripotiwa kutoka maeneo mengine ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki, ambayo katika uchaguzi mkuu uliopita ilishuhudia maafa makubwa.

Uhuru Kenyatta akipiga kura yake katika kituo cha skuli ya msingi ya Mutomo, kaskazini mwa Nairobi hapo tarehe 4 Machi 2013.
Uhuru Kenyatta akipiga kura yake katika kituo cha skuli ya msingi ya Mutomo, kaskazini mwa Nairobi hapo tarehe 4 Machi 2013.Picha: Getty Images

Kenyatta anakabiliwa na mashitaka kwenye mahakama ya ICC, ambako anatuhumiwa kusaidia katika uchochezi wa ghasia za baada ya uchaguzi hapo mwaka 2007-2008 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa.

Marekani na mataifa mengine ya Ulaya yameonya juu ya "matokeo mabaya", ikiwemo mataifa hayo kulazimika kukata mawasiliano na Kenyatta atachaguliwa kuwa rais, kwa sababu ya kukabiliwa kwake na kesi hiyo mbele ya ICC.

Mara baada ya Rais Mwai Kibaki kutangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2007, wafuasi wa Odinga waliingia barabarani, hatua ambayo ilianzisha miezi miwili ya mashambulizi ya kikabila. Mbali ya zaidi ya watu 1,000 kuuawa, wengine zaidi ya 600,000 walilazimishwa kuyahama makaazi yao.

Maafisa wa serikali wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha kwamba kiwango kama hicho cha ghasia hakirejelewi mara hii, huku wagombea wote wawili wakuu - Odinga na Kenyatta - wakiahidi kukubaliana na matokeo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdulrahman