Kansela Angela Merkel ameanza mazungumzo rasmi ya kuunda serikali | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kansela Angela Merkel ameanza mazungumzo rasmi ya kuunda serikali

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana matumaini wakati alipokuwa akiingia katika mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali ya mseto na viongozi wa chama cha Social Democratic SPD

Kansela Angela Merkel amesema wanatarajia kwenda  mbele katika jitihada zao za kuunda serikali na ndio maana ana matumaini juu ya majadiliano hayo huku akisema  anaamini hilo linaweza kufikiwa kwa wakati. Miezi minne baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani bado hakuna  serikali mpya. Iwapo mazungumzo na chama cha Social Democratic yatafanikiwa serikali hiyo mpya inatakiwa kukamilika ifikapo wakati wa Pasaka.

"Siku 14 zilizopita tulikamilisha mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali, ni vizuri kwamba leo tunaweza kuanza mazungumzo hayo, lazima tujadiliane wazi ni mambo gani mema yanafaa kwa Ujerumani ya siku za usoni, tutahakikisha kuwa tunajadiliana haraka ili kupata matokea kwa wakati;"alisema Merkel alipokuwa nje ya makao makuu ya chama cha CDU mjini Berlin. 

Kwa upande wake kiongozi wa chama cha Christian Sociol Union CSU Horst Seehofer, amesema chama chake kinaingia katika majadiliano kwa moyo mkunjufu lakini akasema huenda majadiliano hayo yasifanikiwe iwapo kilichoafikiwa kitakataliwa na wanachama wa Social Democrat.

Kiongozi wa SPD Martin Schulz anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa chama chake kuingia upya katika serikali

ya muungano iliyoiongoza Ujerumani tangu mwaka 2013.

Vyama hivyo vitatu  yani  vyama ndugu  vya kihafidhina  Christian Democratic Union  CDU na Christian Social Union CSU, pamoja na chama cha SPD wana nia ya kumaliza majadiliano hayo ndani ya wiki mbili ambapo baadaye mpango watakaoafikiana utapelekewa wanachama wa SPD ili kuidhinishwa.

Lakini bado kuna wasiwasi wa Ujerumani kurejea tena katika uchaguzi  mpya iwapo majadiliano hayo hayatafua dafu.

Hata hivyo Kansela huyo wa Ujerumani wa muda mrefu alijaribu kuunda serikali na chama cha walinzi wa mazingira die Grüne na waliberali  wanaowapendelea bishara chama cha  Free Democrats jaribio ambalo lilishindwa mwaka uliopita.

Chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU, chama cha Bavaria CSU na chama cha Social Democrats wote walifanya vibaya katika uchaguzi uliyofanyika mwezi Septemba mwaka jana hatua ambayo ilikipa chama cha cha siasa kali cha AFD kinachopinga uhamiaji kujipatia umaarufu.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com