Jumuiya ya Kimataifa ina wasiwasi na Burundi | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jumuiya ya Kimataifa ina wasiwasi na Burundi

Wakati hali bado ikiwa tete kote nchini Burundi;Jumuiya ya Kimataifa imezungumzia wasiwasi wake juu ya hali inayoshuhudiwa kwa hivi sasa katika taifa hilo,huku hatma ya uongozi wa nchi hiyo ikiwa bado ni kitendawili

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Marekani imezitaka pande zote kumaliza vita mara moja na kuvumiliana wakati mgogoro huo ukitafutiwa Ufumbuzi.

Wizara ya mambo ya nje ya Mareakani kupitia msemaji wake Jeff Rathke imetoa mwito kwa pande zote zinazohusika na ghasia Burundi kukomesha vurugu hizo na kujenga hali ya kuvumiliana ingawa wakati huohuo msemaji huyo hakuweza kuthibitisha ikiwa kilichotokea burundi ni mapinduzi au la.Hadi wakati huu Uongozi wa Burundi unalipuuza tangazo la aliyekuwa mkuu wa ujasusi bwana Niyombare anayeshikilia kwamba kwasasa hakuna serikali madarakani bali rais amepinduliwa madarakani.

Wananchi washangilia mapinduzi Bujumbura

Wananchi washangilia mapinduzi Bujumbura

Katika mtandao wa Face book upande wa rais Nkurunzinza umedai jaribio la mapinduzi limegonga mwamba ingawa pia hakuna anayefahamu hasa aliko rais Nkurunzinza hadi kufikia jana usiku.Viongozi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokutana Daresalam Tanzania wamelaani jaribio hilo la kutaka kumuondoa madarakani rais Nkurunzinza lakini na kutaka kurudishwa kwa sheria.Kwa upande mwingine Marekani pia imezungumzia wasiwasi wake kuhusiana na wanamgambo kupewa silaha ingawa chama tawala CNDD-FDD kimeyapinga madai hayo.

Jijini New-York ambako Juhudi za kuutafutia suluhu mgogoro huu zinategemewa kuanza hii leo kwa kikao maalum cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,tayari wanadiplomasia wamesema baraza hilo la usalama limeijadili Burundi wakati wa chakula cha mchana jana Jumatano pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye binafsi amezitaka pande zote zinazovurugana kuwa watulivu na kujizuia na ghasia.

Wapinzani ndani ya Burundi wanasema azma ya rais Nkurunzinza ya kutaka kugombea muhula wa tatu inakiuka katiba na makubaliano ya arusha yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006 ingawa Mahakama ya Katiba ya taifa hilo ilitoa uwamuzi tofauti uliomruhusu Nkurunzinza kugombea.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi wake kwa kuzingatia hoja kwamba kipindi cha kwanza cha uongozi wa Nkurunzina alichaguliwa na bunge na sio kupitia kura za wananchi,lakini wakosoaji kwa upande mwingine wanasema mahakama hiyo imepitisha uamuzi wake kwa kupendelea upande mmoja.Kutokana na utata huo na maji kuzidi unga wafadhili wa Kimataifa ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya wanaukosoa msimamo wa Nkurunzinza wa kutaka kugombea tena.

Rais Pierre Nkurunziza akihutubia wajumbe wa CNDD FDD Bujumbura tarehe 25.04

Rais Pierre Nkurunziza akihutubia wajumbe wa CNDD FDD Bujumbura tarehe 25.04

Umoja wa Ulaya na mkoloni wa zamani wa Burundi Ubelgiji zimesema zinafuta sehemu ya msaada wake na hasa msaada wa kusimamia shughuli za uchaguzi kufuatia vurugu zinazoendelea. Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya warundi 70,000 wamekimbilia kwenye nchi jirani katika eneo hilo lenye historia ya mapigano ya kikabila.

Juu ya hilo hakuna anayefahamu nini mustakabali wa Burundi kwa sasa hasa ikizingatiwa utata uliopo kuhusu kile kinachoonekana kuwa mapinduzi na kutofahamika alipo rais Nkurunzinza,ambaye jaribio lake la kutaka kurudi nyumbani jana kutoka Tanzania lilizuiliwa na wapinzani wake wanaosemekana wanaudhibiti uwanja wa ndege na kuamrisha mipaka yote kufungwa.Mwandishi wa shirika la habari la Afp amethibitisha pia kwamba uwanja wa ndege wa Bujumbura uko mikononi mwa vikosi vya wanaounga mkono mapinduzi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com