1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lawakamata "wapiganaji wa Hamas" hospitali

15 Februari 2024

Vikosi vya jeshi la Israel (IDF) leo vimewakamata watu kadhaa vilipoivamia hospitali kuu ya mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.

https://p.dw.com/p/4cRac
Hospitali ya Nasser
Kifaru cha Israel kikiondoka kutoka hospitali ya Nasser, huko Khan Younis Picha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema vikosi vya nchi hiyo vilifanya operesheni mahsusi katika hospitali ya Nasser iliyokuwa na lengo la kuwakamata wapiganaji wa kundi la Hamas.

Amesema miongoni mwa waliokamatwa ni wale waliohusika na shambulizi la Oktoba 7 mwaka jana dhidi ya Israel. IDF haijatoa idadi ya waliokamatwa kwenye operesheni hiyo iliyosababisha kifo cha mgonjwa mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya askari wa Israel kufyetua risasi.

Hapo kabla msemaji wa wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na kundi la Hamas alithibitisha uvamizi huo na kuelezea kwamba moja ya kuta za majengo ya hospitali ya Nasser imeharibiwa baada ya wanajeshi wa Israel kuingia kwa kishindo. 

Kwa mujibu wa Israel tathmini ya kijasusi iliyofanyika inaonesha zaidi ya asilimia 85 ya majengo ya hospitali za Ukanda wa Gaza yanatumika kwa operesheni za kundi la Hamas.

Mara kadhaa jeshi la nchi hiyo limeripoti kugundua mahandaki, silaha na hata kamandi za kundi la Hamas chini ya majengo ya hospitali madai ambayo maafisa wa hospitali hizo wamekuwa wakiyakanusha.

Uvamizi kwenye hospitali hizo umekuwa ukifanya uharifu mkubwa na wakati mwingine kulazimisha huduma za matibabu zinazohitajika sana Ukanda wa Gaza kusimama kwa siku kadhaa.

Gaza itahitaji mpango wake wa "Marshall" kutokana na uharibifu uliotokea 

Kwa ujumla sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza imebakia magofu matupu. Vikosi vya Israel vimekuwa vikivurumisha mfululizo makombora na mabomu tangu kuanza kwa operesheni yake Oktoba mwa jana kujibu shambulizi la kutisha lililofanywa na kundi la Hamas.

Hali ya kibanadaamu Gaza
Vita vimewalazimisha wakaazi wa Gaza kuishi maisha taabu.Picha: MAHMUD HAMS/AFP

Hii leo mkuu wa shirika la biashara la Umoja wa Mataifa amesema Gaza itahitaji mpango unaofanana na ule wa "Marshall" ambao uliandaliwa na Marekani kuyapiga jeki mataifa ya Ulaya baada ya vita vikuu vya pili vya dunia. 

Richard Kozul Wright ameuambia mkutano mmoja wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba uharibifu uliotokea Gaza hivi sasa tayari umepindukia mara nne ya ulioshuhudiwa kwenye vita vya wiki saba kwenye Ukanda vya mnamo mwaka 2014.

Amekadiria kwamba alau dola bilioni 20 za kimarekani zitahitajika kuijenga upya Gaza. Amesema kiwango hicho lakini ni iwapo vita vinavyoendelea vitasimama hivi sasa.

Mawaziri wa Israel wapinga tetesi za mpango wa kuundwa dola ya Palestina 

Wapalestina wakipeperusha bendera ya Palestina
Suala la kuundwa taifa huru la Palestina ni kizingiti kikubwa katika kuumaliza mzozo wa Mashariki ya KatiPicha: Emmanuele Contini/IMAGO

Katika hatua nyingine mawaziri waandamizi wa serikali ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wametangaza upinzani wao kuhusu kuundwa taifa huru la Palestina wakisema kamwe hawatakubali mpango wa aina hiyo wanaodai ni kitisho cha kuwepo taifa la Israel.

Matamshi yao yanafuatia ripoti ya gazeti la Washington Post la nchini Marekani iliyosema kwamba utawala wa rais Joe Biden unafanya kazi na mataifa ya kiarabu ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Saudi Arabia kuandaa mpango wa baada ya vita unaojumuisha tarehe na muda rasmi wa kuundwa dola ya Palestina.

Mawaziri hao akiwemo anayehusika na masuala ya fedha,  Bezalel Smotrich, wamesema daima hawatauridhia mpango huo utakaowapatia Wapalestina kile wamekitaja kuwa zawadi "hata baada ya kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya Israel."

Mataifa kadhaa ya magharibi yakiongozwa na Marekani yanapigia debe suluhisho la kuundwa madola mawili kama njia ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati.

Maafisa wa Palestina nao wamekwishasema kwamba hakutakuwa na mafanikio yoyote iwapo suala la kuundwa dola huru la Wapalestina halitakuwa msingi wa juhudi za kisiasa za kuutanzua mzozo uliopo.