1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, vita dhidi ya madawa ya kulevya vitaitakasa Tanzania?

22 Februari 2017

Zaidi ya vijana 1,000 wa Kitanzania wanaripotiwa kutiwa hatiani kutokana na madawa ya kulevya katika nchi mbalimbali, 68 wakisubiri kunyongwa na huku ndugu zao wakibakia kupokea habari hizo kwa machungu makubwa.

https://p.dw.com/p/2Y27b
Italien Militär baut Cannabis für Schwerkranke an
Picha: Getty images/AFP/F. Monteforte

"Ukishikwa na madawa ya kulevya, ubebe msalaba wako mwenyewe," anaapiza Rais John Magufuli wa Tanzania ambaye anasema amedhamiria kupambana na tishio la madawa hayo mpaka mwisho.

Kuhusu Watanzania waliofungwa nchi za nje kwa hatia za madawa hayo, anasema masikitiko yoyote kwamba "Yeyote atakayehukumiwa kunyongwa, akanyongwe huko huko."

Wakati huo huo, kiongozi huyu aliyejizolea sifa na ukosowaji kwa hatua na kauli zake za haraka haraka, ameshawaagiza mabalozi wa Tanzania walio nchi za nje wasijihusishe kabisa na kesi za Watanzania wanaokamatwa kwa madawa ya kulevya.

Hasira za Rais Magufuli dhidi ya wasafirishaji pamoja na watumiaji wa madawa ya kulevya zinaonekana wazi kwenye maneno yake na kiapo chako ni kwamba "mapambano dhidi ya madawa hayo hapana budi yashinde".

Lakini je, ushindi upo kweli njiani? 

Huko nyuma, Watanzania wengi walidhani kuwa ushindi dhidi ya madawa ya kulevya haufikiriki kwa jinsi ambavyo makundi ya wauzaji yanaongezeka kwa nguvu nchi nzima.

Matumizi pamoja na biashara ya siri ya madawa haya haramu kwa miaka mingi yalipelekea maelfu ya vijana wa kiume na wa kike kujiangamiza wenyewe, familia zikasambaratika, watoto wakakosa haki yao ya elimu ya msingi na baadhi ya maeneo nchini yakawa hayaingiliki kwa sababu ya vurugu na uhalifu kutokana na madawa.

Vita vya chini kwa chini havikufanikiwa

Tansania John Magufuli
Rais John Magufuli anasema serikali yake haitawasaidia Watanzania wanaokabiliwa na tuhuma za biashara na matumizi ya madawa ya kulevya nje ya nchi hiyo.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Hapa na pale na chinichini, watu walitaja majina ya walioshukiwa ama kuuza "unga" au kuwa walaji, lakini watawala hawakuwa na nguvu kuchukua hatua. Matokeo yake kila mtu akakata tamaa.

Tuhuma ya wengi ilikuwa kwamba wakubwa ama wanashirikiana na vigogo wa madawa ya kulevya au waliogopa visasi, ambavyo vingewashukia kama radi. Ni jambo la kusikitisha kwamba hali hii ilionesha ukosefu mbaya wa imani kati ya raia na serikali.

Taarifa zilieleza kuwa wauza madawa wamelimbikiza mali na wana ushawishi mkubwa, wana ubia na masoko ya magendo ya kimataifa ambako kazi yao ni kusambaza na kuuza kokeine, heroini na aina nyingine za madawa ya kulevya barani Afrika na nje.

Bangi ni mmea ambao unaoteshwa nchini na hutumika katika baadhi ya mikoa kama dawa, mboga ya majani na kiburudisho. Hivi karibuni bangi imegeuzwa kienyeji kuwa zao la biashara linalotegemewa na baadhi ya jamii.

Kilimo haramu cha bangi kimekuzwa na fursa yake ya kuwapatia watu pesa za kijikimu katika mazingira magumu kiuchumi, Katika wilaya ya Muleba kaskazini magharibi mwa Tanzania wakulima wamekamatwa hivi karibuni na kushtakiwa kwa kutumia mbolea iliyotolewa na serikali kukuza bangi badala ya mazao ya chakula.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Madawa ya Kulevya na Uhalifu inasema kuwa Afrika inazidi kuleta wasiwasi  kutokana na kukamata dawa za heroini na bara hili linazidi kutumika kama njia muhimu ya kupitisha madawa ya kulevya.

Ushindi dhidi ya madawa hayo ni muhimu kwa Tanzania hasa wakati ambapo uchumi wake haujawa imara, madhara ya hali mbaya ya hewa hukausha akiba walizojiwekea watu na uhaba wa chakula unakuwa mkali.

Ili kuokoa uchumi usiporomoke, serikali inahitaji kutumia nguvu kazi zake zote katika shughuli za uzalishaji. Ndiyo sababu Rais Magufuli anaendesha mapambano yanayolenga sehemu nyingi dhidi ya madawa ya kulevya na ufisadi nchini Tanzania.

"Tukichukua jambo hili kimzaha, taifa letu litapoteza sehemu kubwa ya nguvu kazi," anaonya Rais Magufuli, akisisitiza kuwa vijana Watanzania wakombolewe kutokana na madawa ambayo yamewapotezea ndoto zao kuhusu maisha ya baadaye.

Madawa ya kulevya hubeba uhalifu mwengine

Sansibar Stonetown Heroinsüchtige  Sober House
Vijana wakiwa kwenye kituo cha kuwasaidia waathirika wa madawa ya kulevya visiwani Zanzibar.Picha: DW/M. Hartlep

Duru zenye taarifa za kuaminika zinasema kuwa biashara ya madawa ya kulevya imeambatana na utakatishaji wa fedha haramu Tanzania kwa kipindi kirefu. Wauzaji hudanganya kuhusu vyanzo vya fedha zao kupitia mihamala ya benki na maduka ya fedha za kigeni.

Vita dhidi ya madawa sasa imeathiri kiasi cha fedha taslimu zipitazo katika benki, vimeeleza vyanzo vya kibenki. Vile vile huenda athari hizo zikabainika karibuni au baadaye katika soko la hisa.

Inahofiwa kuwa mapato haramu kutokana na madawa ya kulevya huwapa nguvu baadhi ya wawekezaji katika soko la hisa, hutumika kama hongo kwa watumishi wa umma na hurahisisha kampeni za baadhi ya wanasiasa wakati wa uchaguzi.

Vita vya Tanzania vitaleta matokeo mazuri kama vitaendelea zaidi ya kuwawinda washukiwa wadogo na kuwakamata wakubwa wa usafirishaji wa madawa na wakala wao, baadhi yao wakiwa na mahusiano na wahimizaji wa sheria ikiwa pamoja na askari wa magereza.

Wengi wa vijana Watanzania waliofungwa nchi za nje kutokana na hatia za madawa ya kulevya ni wahanga wa safari za vipofu. Walipumbazwa kuwa wachukuzi wa madawa kutokana na shauku yao ya kusafiri nchi za nje ili wapate pesa kirahisi.

Wamefungwa Msumbiji, Iran, Nepal, India, Uchina, Uturuki, Ugiriki, Afrika Kusini, Brazil, Malaysia, Thailand, Indonesia, Ngazija, Pakistan, Japan, Nigeria, Ghana, Uingereza, Kenya, Misri na Uganda.

Serikali, hata hivyo, itasifiwa zaidi ikifanya mara kwa mara uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya madawa ili itambue madhara yake katika jamii, kwa nini raia wanatumia madawa au wanakuwa wauzaji wa madawa hayo. Kuhimiza sheria peke yake hakutoshi kitu. 

Mwandishi: Anaclet Rwegayura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef