Je, Ronaldo atatamba tena? | Michezo | DW | 26.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Je, Ronaldo atatamba tena?

Mabingwa wa Ulaya Ureno siku ya Jumatatu watakuwa wanapimana nguvu na Uholanzi huko Uswisi. Ureno waliwalaza Misri mbili moja katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki waliyoicheza Ijumaa.

Kocha wa Ureno Fernando Santos amesema mechi hii ni muhimu sana na ni matayarisho yanayohitajika kwa timu yake.

"Hakuna timu nyingi ambazo zinaweza kulinganishwa na Uholanzi kwasababu Uholanzi siku zote imekuwa na inasalia kuwa timu nzuri iliyo na wachezaji wazuri," alisema Santos. "Tuliichagua wakati tulipokuwa tunachagua mechi zetu za kirafiki kwasababu tulikuwa tunataka timu itakayotupa ushindani, tulikuwa tunataka kujitayarisha vyema na hiyo ndiyo sababu ambayo ilitufanya tucheze na Misri pia," aliongeza kocha huyo wa Ureno.

Uholanzi wao hawakufuzu kwenye kombe la dunia huko Urusi na kwenye mechi yao ya kwanza ya kirafiki walifungwa moja bila na England mjini Amsterdam. Kocha wao Ronald Koeman amesema wanacheza mechi hizi za kirafiki licha ya kuwa hawatosafiri kwenda Urusi kwasababu wana malengo.

Uhispania na Argentina watatoana jasho Madrid

"Lengo letu ni kushiriki katika mashindano ya Euro ya mwaka 2020 na nafikiri kucheza na Ureno ni hatua nzuri kwasababu ni timu bora na inatupa nafasi ya kuufanya mchezo wetu kuwa bora ikilinganishwa na jinsi tulivyocheza dhidi ya England," alisema Koeman.

Mechi ambayo Uholanzi walicheza na England ilikuwa ya kwanza kwa Ronald Koeman kama kocha wa hao the Orange.

Na huko Madrid nyasi zitawaka moto kesho kwani Uhispania ambao ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upatu watakuwa wanatoana jasho na Argentina katika uwanja wa klabu ya Atletico Madrid, Wanda Metropolitano.

Fussball Freundschaftsspiel - Deutschland vs Spanien Tor 0:1 (Reuters/T. Schmuelgen)

Wachezaji wa Uhispania wakisherehekea goli lao dhidi ya Ujerumani Alhamis

Uhispania watawakosa wachezaji wao David Silva na Gerard Pique kwa kuwa Silva ameondoka kwenye kambi ya mazoezi kwasababu za kibinafsi huku Pique akiwa anauguza jeraha la goti. Kukosekana kwa Silva na uwezekano wa kuwa Andres Iniesta huenda akapumzishwa katika mechi hiyo kunaweka shinikizo kwa kiungo wa Real Madrid Isco ambaye aling'ara sana Uhispania walipoutawala mchezo kwa kipindi cha nusu saa ya kwanza kwenye ile mechi yao ya kirafiki na Ujerumani Alhamis walipotoka sare ya bao moja.

Ufaransa watatafuta ushindi kwa Urusi huko Moscow

Lionel Messi hakushiriki mechi ya kwanza ya kirafiki Argentina walipowalaza Italia magoli mawili kwa nunge na kuna taarifa zinazosema kwamba mchezaji huyo wa Barcelona ni majeruhi na kocha Jorge Sampaoli hatomshirikisha mechi ya kesho pia ingawa mshambuliaji Sergio Aguero huenda akacheza.

Ufaransa watakuwa wanaelekea Moscow kutafuta ushindi dhidi ya wenyeji Urusi baada ya kushangazwa na Colombia katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki walipocharazwa magoli matatu kwa mawili. Ufaransa wana wachezaji wachanga na wenye talanta kikosini mwao na ni mojawapo ya timu ambazo zinatarajiwa kufika mbali kwenye kombe la dunia Urusi.

Fußball Länderspiel Deutschland vs Frankreich | Tor (Reuters/W. Rattay)

Mshambuliaji wa Ufaransa Alexander Lacazette akisherehekea baada ya kufunga

Baada ya ushindi wao wa moja bila dhidi ya Uholanzi England watakuwa wanatafuta kuendeleza mchezo wao bora watakapokuwa wanacheza na Italia kesho uwanjani Wembley. Hiyo itakuwa mechi ya pili kwa kocha wa Italia wa muda Luigi Di Biagio.

Mlinda lango Gianluigi Buffon mwenye umri wa miaka 40 anatarajiwa kupumzishwa na nafasi yake ichukuliwe na chipukizi Gianouigi Donnarumma mwenye umri wa miaka 19. Buffon ndiye aliyekuwa langoni katika mechi ya Italia na Argentina wiki iliyopita.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/Reuters/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman