Malengo ya Donald Trump kuhusu Iran: Nini kinaweza kufikiwa?
1 Machi 2026
Baada ya Israel kufanya ilichokiita "mashambulizi ya kujihami” dhidi ya Iran Jumamosi asubuhi, Rais Donald Trump alitangaza katika hotuba kwamba "operesheni kubwa za kijeshi” za Marekani pia zilikuwa zinaendelea.
"Lengo letu ni kuwalinda wananchi wa Marekani kwa kuondoa vitisho vya dhahiri kutoka kwa utawala wa Iran,” Trump alisema katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, akiapa kuharibu uwezo wa nyuklia na kijeshi wa Iran.
Akieleza malengo ya kampeni hiyo, Trump pia alisema Marekani ingeharibu kabisa mpango wa makombora ya masafa marefu wa Iran na vikosi vyake vya majini.
Kwa kuwa kampeni ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran haionekani kuwa ya muda mfupi, wachambuzi wanaamini kuwa mzozo huu huenda ukaendelea kwa wiki kadhaa, kama sio miezi.
Lengo la 1: Kuizuwia Iran kupata au kutengeneza silaha za nyuklia
Baada ya vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mnamo Juni 2025, Trump alitangaza kwamba Marekani ilikuwa imeangamiza kabisa vituo vikuu vya nyuklia vya Iran na kwamba Jamhuri hiyo ya Kiislamu isingeweza kutengeneza silaha za nyuklia katika siku za usoni.
Marcus Schneider, mtaalamu kutoka wakfu wa Friedrich-Ebert nchini Lebanon, anasema anadhani Marekani kufanya vita vingine vyenye lengo la kuharibu silaha za nyuklia za Iran, kwa sehemu kubwa ni kisingizio tu.
Katika mahojiano na DW, mtaalamu huyo anasema katika mashambulizi ya awali ya Marekani, mpango wa nyuklia wa Iran ulirudishwa nyuma kwa miezi au miaka michache kulingana na baadhi ya wachambuzi, lakini hauwezi kuangamizwa kikamilifu.
Anasema suala hilo ni la utaalamu, na kwamba Iran tayari inao utaalamu wa kutengeneza vinu vya nyuklia na kurutubisha madini ya urani, na utaalamu huo hauwezi kuondolewa kwa mashambulizi ya anga.
Shahin Modarres, mchambuzi wa masuala ya usalama anaeishi nchini Italia, pia ameiambia DW kuwa kuzuia uundaji wa silaha za nyuklia ni lengo la kimkakati, na sio la sera tu. Hata hivyo, Modarres anaafiki kuwa Iran yenye silaha za nyuklia mara zote haitakubalika machoni pa Israel na Marekani.
Diba Mirzaei kutoka Taasisi ya Ujerumani ya Masomo ya Kimataifa na Kikanda (GIGA) analiita suala hilo "kisingizio cha kuhalalisha vita,” akisema kuwa "kwa sasa hakuna hatari ya wazi inayotoka Iran.”
Mazungumzo kati ya Marekani na Iran mjini Geneva wiki hii kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran hayakuzaa matunda yoyote.
Lengo la 2: Kufuta kabisa mpango wa makombora ya balistiki ya Iran
Wataalamu wanasema Marekani na Israel wanauchukulia mpango wa makombora wa Iran kuwa wenye hatari zaidi hata kuliko ule wa silaha za nyuklia, hususan baada ya uwezo iliouonyesha Iran katika vita vya siku 12 vya katikati ya mwaka jana, ambapo iliweza kupiga shabaha ndani ya Israel na kuharibu vituo vya kijeshi vya Marekani.
Modarres kutoka taasisi ya GiGa anasema ingawa viwanda vya kuunda makombora na mnyororo wa usambazaji wake vinaweza kushambuliwa, utaalamu wa kiufundi hauwezi kuharibiwa, na kwa hivyo, suala la kufuta kabisa mpango wa makombora wa Iran haliwezekani, ingawa unaweza kudhoofishwa.
Lengo la 3: Kuharibu vikosi vya majini vya Iran
Schneider kutoka wakfu wa Friedrich-Ebert anakubaliana na mtazamo huo, kwa kusema viwanda vya makombora vya Iran ni raslimali ya ndani ya nchi, na kwa hivyo, hata kama shehena iliyopo itaharibiwa, inaweza kujengwa tena. Suali pekee ni muda utakaochukua ujenzi huo, na gharama ya kibinadamu.
Kwa Schneider, inawezekana zaidi kwa Marekani kuharibu jeshi la majini la Iran kuliko kuharibu uwezo wake wa makombora. Anaongeza pia kuwa ni muhimu kuelewa kwamba Iran ina boti ndogo nyingi na hadhani kama hilo ni jambo linaloweza kufanikiwa kwa wiki moja.
Sara Kermanian, mtafiti wa masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Sussex, pia anaamini Marekani inaweza kudhoofisha pakubwa vikosi vya majini vya Iran katika muda mfupi, na kupunguza uwezo wao wa kuvuruga usafiri baharini.
Lengo la 4: Kuangusha utawala wa Iran
Haijulikani wazi jinsi Rais Trump anavyokusudia kufanikisha lengo la kuangusha utawala wa Iran kupitia kampeni yake hii mpya, kwa kuwa Washington haijatoa dalili ya kuanzisha operesheni ya ardhini ndani ya Iran. Lakini ripoti za mashambulizi ya anga ya Israel na Marekani kwenye malengo ya kijeshi na ya kiserikali ndani ya Iran zinaonyesha kuwa kampeni inalenga kudhoofisha utawala huo kwa kiwango kikubwa.