1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je hatua mpya za kupambana na ugaidi Sahel zinajitosheleza?

Lilian Mtono
14 Januari 2020

Ufaransa na mataifa matano ya ukanda wa Sahel ama G5 yametangaza kuimarisha ushirikiano kwenye vita dhidi ya ugaidi katika ukanda huo unaokabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo.

https://p.dw.com/p/3WBa9
Frankreich G5-Sahel Gipfel in Pau
Picha: DW/F. Tiassou

Kwenye mkutano wa kilele wa mataifa hayo ya G5, Ujumbe ulikuwa ni wa wazi. Rais wa Burkina Faso na mwenyekiti wa sasa wa mkakati wa mataifa hayo matano ya SahelRoch Marc Christian Kabore alisema kunahitajika matokeo ya haraka kwa sababu bado kuna kitisho cha kukosekana kwa imani miongoni mwao. Alisema wanahitaji kudhihirisha uwezo wao wa kukabiliana na changamoto hiyo.

Rais Kabore alikuwa akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pau kusini mwa Ufaransa.

Mkutano huo unafuatia mwaliko wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa mataifa hayo ya G5 ambayo ni Mali, Burkina Faso, Niger, Chad na Mauritania. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kutangaza hatua mpya za kuimarisha vita vyao dhidi ya ugaidi kwenye ukanda huo.

Hali ya usalama inazidi kuzorota kila uchwao kufuatia kuongezeka mashambulizi. Kati ya Januari na Novemba mwaka jana, zaidi ya raia 1,500 waliuawa na milioni moja waliyakimbia makazi yao. Idadi hiyo ni mara mbili ya wale waliokimbia mwaka jana, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa. Shambulizi la hivi karibuni Januari 9 katika mji wa Chinegodar kaskazini mwa Niger lilisababisha vifo vya wanajeshi 89.

Frankreich l Macron wirbt für Sahel-Initiative
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anakabiliwa na ukosoaji mkali kuhusiana na wanajeshi wake waliopo Sahel.Picha: Getty Images/AFP/G. Horcajuelo

Ni kutokana na hali hiyo sasa Ufaransa na mataifa ya G5 yametangaza kuanzisha mfumo wa ushirikiano wa kijeshi utakaoratibu shughuli za jeshi la Ufaransa lililopo kwenye ukanda huo tangu mwaka 2014, lenye jumla ya wanajeshi 4,500 pamoja na muungano wa majeshi ya G5 yenye jumla ya wanajeshi 5,000. Ufaransa itaongezea wanajeshi wake 220.

Kikosi kipya kinachoitwa Takuba kitaundwa ili kuviunganisha vikosi maalum kutoka nchi nyingine za Ulaya, ambao wataungana na wale ambao tayari wanatoa msaada wa vifaa kutoka mataifa kama Uingereza, Denmark na Ujerumani.

Mkuu wa zamani wa ujumbe wa kijeshi wa Ufaransa na mshauri wa masuala ya kijeshi Jenerali Dominique Trinquand ameliambia shirika la habari la DW kwamba hiyo ni habari njema.

Trinquand anaamini kwamba ukanda wa Sahel unatakiwa kuangaliwa kwa jicho la kipekee katika mapambano dhidi ya ugaidi, na sio tu Ufaransa. Ana wasiwasi kwamba Sahel inaweza kuwa kama Syria hapo baadae na huenda wapiganaji wake wakatumwa kwenye mataifa ya Ulaya kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Burkina Faso Tofalaga 2019 | Operation Barkhane
Wachambuzi wanaamini kwamba Sahel inahitaji wanajeshi kutoka nje kusaidia vita hivyoPicha: picture-alliance/dpa/Maxppp/P. de Poulpiquet

Taarifa ya pamoja ya mkutano huo wa kilele pia ilithibitisha upya nia ya mataifa hayo ya Sahel kushirikiana kijeshi na Ufaransa katika eneo hilo lakini pia nia ya kuimarisha uwepo wa majeshi ya kimataifa, suala ambalo Macron amelihimiza wakati akiwaomba wakuu wa mataifa kuachana na mawazo yenye utata kuhusu uwepo wa majeshi ya Ufaransa kwenye eneo hilo.

Kundi la waandamanaji lililokuwa kama mita 600 hivi kutoka kasri kuliofanyika mkutano huo, wanapinga uwepo wa wanajeshi hao. Abdoulaye Adouwal aliyetokea mji mkuu Paris ameiambia DW kwamba anataka vikosi vya Ufaransa viondoke. Anadai kwamba viongozi wao wameleta wanajeshi wa nje wakidai watarejesha usalama, lakini bado mashambulizi yanaendelea. Wanasema ni bora wangewapa mafunzo ya kijeshi vijana wa nchi zao ili warejeshe amani za nchi zao wenyewe.

Mtafiti mwandamizi kwenye taasisi ya masomo ya usalama nchini Ivory Coast William Assanvo anaielewa ghadhabu hiyo, ingawa anaamini kwamba bila ya wanajeshi hao wa Ufaransa hali ingekuwa mbaya zaidi. Anasema, ni wazi G5 wanahitaji msaada.

Lakini pamoja na yote bila ya kuwepo mikakati mipya ya kupambana na ugaidi kwenye ukanda wa Sahel, kuna wasiwasi kwamba miito ya vikosi hivyo kuondoka itaongezeka.