Israel yakosolewa vikali kwa kuwafukuza Wapalestina | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Israel yakosolewa vikali kwa kuwafukuza Wapalestina

Marekani yaiongoza jumuiya ya kimataifa kuikosoa Israel

default

Hillary Clinton

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeikosoa vikali Israel kwa kuzifukuza familia za Wapalestina kutoka eneo la Jesusalem Mashariki zikionya kuwa hatua za aina hiyo zinahatarisha mchakato wa kusaka amani ya Mashariki ya Kati. Umoja wa Ulaya pia umesema ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika eneo hilo unakiuka sheria za kimataifa.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton ameiongoza jumuiyaya kimataifa kulaani kufukuzwa kwa familia za Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki akiileza hatua hiyo kuwa kitendo cha kujutia na cha ochokozi. Bi Clinton pia ameishutumu Israel kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ya kimataifa kwa mujibu wa mikataba ya amani iliyotiwa saini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington Marekani akiwa ameandamana na waziri wa kigeni wa Jordan, Nasser Judeh, bi Clinton ameelzea masikito yake makubwa kusuhu kufukuzwa Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki.

"Vitendo hivi ni vya kujutia sana. Nimeshawahi kusema kuwa kuzifukuza familia na uvunjaji wa makaazi huko Jerusalem Mashariki si njia ya Israel kutimiza majukumu yake. Nimeitaka serikali ya Israel na maafisa wa baraza la mji wa Jerusalem wajiepushe na vitendo vya uchokozi."

Polisi wa kupambana na ghasia wa Israel waliokuwa na virungu walizitimua familia mbili za Wapalestina kutoka nyumbani kwao katika eneo linalokaliwa la Jerusalem Mashariki Jumapili iliyopita, hatua iliyozusha machafuko katika kitongoji cha Sheikh Jarrah, kinachokaliwa na Waarabu. Sheikh Jarra ndicho kitongoji tete kabisa kilichoko karibu na mpaka unaolezwa kuwa wa kijani kati ya mashariki na magharibi mwa Jerusalem.

Hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa mahakama kuu ya Israel kuamuru Wapalestina 53 wafukuzwe kutoka eneo hilo wakiwemo watoto 19.

Sweden, inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka eneo la Jerusalem Mashariki kunakoendelea, ikisema hakukubaliki na ni kinyume cha sheria za kimataifa. Taarifa ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa mjini Brussels Ubelgiji imesema kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki kunaenda kinyume na miito iliyotolewa na jumuiya ya kimataifa kuepukana na vitendo vya uchokozi katika eneo hilo. Taarifa hiyo aidha imesema kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki kunathibitisha mkondo wa kutia wasiwasi unaofuja kuundwa kwa mazingira yanayofaa kuendeleza juhudi za kutafuta suluhisho la mzozo kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Nchi mbalimbali wanachama wa Umoja wa Ulaya pia binafsi zimeikosoa Israel kwa kuwafukuza Wapalestina kutoka eneo la Jerusalem Mashariki. Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Ufaransa, Romain Nadal, amesema kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, hatua ya Israel sio halali na kuongeza kuwa kuwafukuza Wapalestina kunahatarisha mchakato wa kusaka amani.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Norway, Jonas Gahr Stoere, amesema hatua ya Israel inahatarisha mchakato mzima wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Jumuiya ya kimataifa mara kwa mara imehimiza Israel iepukane na vitendo vya uchokozi dhidi ya Wapalestina kwa kuwa hatua hiyo inavuruga uwezekano wa kufikiwa makubaliano kuhusu mji wa Jerusalem kwa msingi wa suluhisho la mataifa mawili.

Israel ililiteka eneo hilo katika vita vyake vya mwaka 1967 vilivyodumu siku sita na baadaye kuligawa katika hatua ambayo jumuiya ya kimataifa haijaitambua. Wapaletina wanataka eneo la Jerusalem Mashariki liwe mji mkuu wa taifa lao huru litakaloundwa ambalo linayajumulisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Hatma ya mji wa Jerusalem ni mojawapo ya maswala nyeti katika mzozo baina ya Israel na Wapalestina.

Mwandishi.Josephat Charo

Mhariri:Aboubakary Liongo

 • Tarehe 04.08.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J3BL
 • Tarehe 04.08.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J3BL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com