1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi yake Ukanda wa Gaza

Josephat Charo
17 Machi 2024

Maafisa wa Palestina wamesema watu kadhaa waliokufa bado wanaaminiwa wamefunikwa chini ya vifusi. Wafanyakazi wa kutoa misaada kila mara hawawezi kuwafikia kutokana na mapigano makali.

https://p.dw.com/p/4dofT
Mapigano makali yameripotiwa katika mji wa Khan Younis
Watu wakitembea kwenye vifusi kufuatia mashambulizi ya kutokea angani ya Israel mjini Khan Younis kusini kwa ukanda wa Gaza.Picha: Yasser Qudih/Xinhua/IMAGO

Mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo ya Israel yamesababisha vifo vya Wapalestina 61. Watu 12 wa familia moja wameuawa baada ya nyumba yao kushambuliwa huko huko Deir al-Balah.

Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema Jumapili kuwa idadi ya vifo tangu kuanza kwa mzozo huo imefikia watu 31,645.

Soma pia: Watu takriban 17 wauwawa katika mji wa Khan Younis

Mapigano makali yameripotiwa katika mji wa kusini mwa ukanda wa Gaza wa Khan Younis na kwingineko. Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameitolea wito Israel kujali ubinadamu na kutoanzisha mashambulizi huko Rafah.