Israel yaendeleza mashambulizi Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Israeli imeendeleza mfululizo wa mashambulizi ya angani katika Ukanda Gaza, huku wanamgambo wa Kipalestina nao wakirusha makombora kuelekea Israeli leo, licha ya miito ya kimataifa ya kutaka usitishwaji mapigano.

Makombora kutoka angani ya yameliangusha jengo jengine kubwa la ghorofa sita ambalo lilikuwa na maktaba na vituo vya elimu vya Chuo Kikuu cha Kiislamu. Picha za vidio zinaonesha madawati, viti vya ofisi, vitabu na waya za kompyuta zilifunikwa kwenye vifusi, huku wakaazi wakifukua vifusi kutafuta mali zao. Soma Mji wa Gaza washambuliwa vibaya na Israel

Wanamgambo wa Kipalestina kwa upande wao wamerusha makombora kadhaa kuelekea Israel, mengine yakiangukia katikati kabisa mwa taifa hilo la Kiyahudi. Soma ZiadiHamas yafyatua zaidi ya maroketi 200 kuelekea Israel

Wapalestina wanaoishi nchini Israel, na maeneo yanayokaliwa kimabavu ya Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi wamefanya maandamano ya pamoja kupinga kile ambacho watetezi wa haki za binaadamu wanachosema ni mfumo wa ubaguzi wa rangi unaodhihirishwa na mashambulizi dhidi ya Gaza.

Mipango ya ksuitisha mapigano

Huku hayo yakijiri, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo Jumanne kujadili jinsi ya kutumia nguvu yao ya kisiasa kusaidia juhudi za kidiplomasia kumaliza mapigano kati ya wanajeshi wa Israeli na wanamgambo wa Kipalestina. 

Licha ya Umoja huo kwa ujumla wake kutoa wito wa kusitisha mapigano na juhudi za kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kumaliza mzozo wa hivi karibuni, lakini mataifa wanachama yamegawanyika juu ya mbinu gani bora ya kusaidia. Soma Jamii ya kimataifa yatoa wito wa amani Israel na Gaza

Umoja wa Ulaya ni mfadhili mkubwa wa misaada kwa Wapalestina, lakini ina ushawishi mdogo juu ya kundi la wapiganaji la Hamas na Israel, licha ya kuwa na mipango ya biashara ambayo inawafaidisha Waisraeli.

Juhudi za kidipolomasia

Leo pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya mkutano wa dharura, huku kukiwa na juhudi za kidiplomasia zinazolenga kukomesha mapigano hayo.

Hata hivyo, hakuna ishara yoyote ya kusitishwa kwa mapigano. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jana Jumatatu alisema nchi yake itaendelea kuwashambulia na kuwalenga wale aliowaita magaidi. Soma Mashambulizi ya jeshi la Israel- yauwa wapalestina huko Gaza

Kulingana na maafisa wa pande zote mbili, jumla Wapalestina 212 wameuawa huko  Gaza, wakiwemo watoto wasiopungua 61, na zaidi ya 1,400 wamejeruhiwa. Kwa upande wa Israel, watu kumi wameuwawa ikiwa ni pamoja na mtoto mmoja, na mamia wamejeruhiwa.

Mapigano ya mara hii yalianza Mei 10 wakati wanamgambo Hamas waliporusha roketi za masafa marefu kuelekea Israel kulipiza kisasi hatua ya vyombo vya usalama vya Isral kuuvamia msikiti mtakatifu wa Al-Aqsa wakati wa siku za mwisho za mwezi wa Ramadhan kukabiliana na maandamano ya Wapalestina wanaopinga kufukuzwa kwa familia kadhaa za Wapalestina kupisha makaazi ya walowezi wa Kiyahudi mjini Jerusalem.

 

Polisi wa Israel wawashambulia Wapalestina kwenye Msikiti wa Al-Aqsa

 

AP/AFP