IS yazidi kupigana licha ya mashambulizi dhidi yake | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

IS yazidi kupigana licha ya mashambulizi dhidi yake

Ushirika unaoongozwa na Marekani umeendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la IS ndani ya Syria na Irak, huku ushirika huo ukinuia kulipiga vita kundi hilo kupitia mtandao wa Intaneti linaoutumia kuvutia wafuasi.

Marekani na washirika wake tayari wamefanya mashambulizi 6,600 dhidi ya kundi la IS.

Marekani na washirika wake tayari wamefanya mashambulizi 6,600 dhidi ya kundi la IS.

Maafisa wa jeshi la Marekani wamesema kuwa wamefanya mashambulizi saba ya anga dhidi ya kundi la IS kati ya Jumapili na jana Jumatatu. Mashambulizi hayo yalijikita nchini Irak, yakilenga ngome za kundi hilo karibu na bwawa la Mosul na katika maeneo ya mji Fallujah ulio kusini mashariki.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Bill Urban amesema mashambulizi haya dhidi ya IS ambayo yalianza Agosti mwaka huu yameigharibu nchi hiyo kitita cha dola milioni 580. Kwa ujumla ndege za Marekani na za washirika wake zimefanya mashambulizi 6,600 dhidi ya IS.

Awali wizara ya ulinzi ya Marekani ilikuwa imesema mashambulizi hayo yanaigharimu dola milioni 7 kwa siku, lakini wachambuzi wa kujitegemea wamesema makadirio hayo ni ya chini.

Mkutano kuhusu wakimbizi wa Syria

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil Elaraby mjini Berlin

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil Elaraby mjini Berlin

Wakati hayo yakijiri Mashariki ya Kati, katika mji mkuu wa Ujerumani- Berlin leo umeanza mkutano wa kuzungumzia suala la wakimbizi wa vita vinavyoendelea nchini Syria. Wawakilishi wa nchi 40 zinazoshiriki katika mkutano huo, wanatafuta jibu kwa changamoto zitokanazo na upungufu wa msaada wa kibinadamu kuwasaidia wahanga wa vita hivyo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kinachohitajika ni kuimarisha mkakati uliopo.

‘‘Hatuna haja ya kubadilisha mtazamo, bali kuimarisha mikakati iliyopo. Hatupaswi tu kuishia katika kuwashughulikia wakimbizi, tunalazimika pia kujihusisha na utangamano wa nchi zinazowapokea wakimbizi hao‘‘. Amesema Steinmeier.

Majira ya baridi kali yanayokaribia ni kitisho kwa wakimbizi kutoka Syria

Majira ya baridi kali yanayokaribia ni kitisho kwa wakimbizi kutoka Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR linakadiria kuwa watu milioni 3 wamekimbia kutoka Syria na kuhamia mataifa jirani, huku wengine zaidi ya milioni 6.5 wakiwa wakimbizi wa ndani ya nchi.

Hakuna msaada kwa wakurdi wa Syria

Nchini Syria kwenyewe mapigano makali yameendelea karibu na mji muhimu wa Kobane ulio karibu na mpaka kati ya Syria na Uturuki. Mwandishi wa shirika la AFP aliye karibu na mji huo amesema wapiganaji wa kikurdi wamekuwa wakipigana kufa na kupona kuwazuia wanamgambo wa IS kusonga mbele wakiukaribia mji huo.

Bado hakuna dalili zozote za msaada ulioahidiwa kwa wakurdi hao; ahadi kwamba wanajeshi wa mamlaka ya wakurdi wa Irak wajulikanao kama Peshmerga wangewasili na zana nziti za kijeshi kuwasaidia wenzao wa Syria bado haijatimizwa. Afisa wa kikurdi amesema msaada huo umekwamishwa na Uturuki, ambayo ilikuwa imekubali kuwapa njia wanajeshi hao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/ DW website

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com