1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya Kobani yamtia mashaka Obama

Admin.WagnerD15 Oktoba 2014

Rais wa Marekani Barack Obama amesema vita dhidi ya kundi la Dola ya Kiislamu IS vinaweza kuchukuwa muda mrefu, na kueleza wasiwasi juu ya namna wapiganaji hao wanavyosonga mbele kwa haraka nchini Iraq na Syria.

https://p.dw.com/p/1DVsH
Barack Obama
Picha: Reuters/G. Cameron

Obama aliyasema hayo wakati wa mkutano wake na wakuu wa majeshi kutoka mataifa 20 washirka katika muungano aliyouunda dhidi ya IS mjini Washington siku ya Jumanne, huku majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani yakizidisha mashambulizi nchini Syria, katika juhudi za kuwasaidia wapiganaji wa Kikurd mjini Kobani.

Lakini rais huyo alikiri kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na hatma ya mji huo uliyoko mpakani mwa Syria na Uturuki. Obama alisema jambo moja lililojitokeza katika mazungumzo yake na wakuu hao wa majeshi ni kwamba hii itakuwa kampeni ya muda mrefu na kwamba hatua za kijeshi pekee hazitaweza kuutatua mgogoro huo.

Ndege za kivita za Marekani za Strike Eagle zikiwa katika operesheni nchini Iraq.
Ndege za kivita za Marekani za Strike Eagle zikiwa katika operesheni nchini Iraq.Picha: picture alliance/dpa/Matthew Bruch

Hatua za kijeshi pekee hazitoshi

"Hii haiwezi kuwa kampeni ya kijeshi tu. Inapaswa kuwa kampeni inayohusisha njia zote. Tunapaswa kufanya kazi bora kuwasiliana maono mbadala kwa wale wanaovutiwa na mapigano nchini Iraq na Syria," alisema rais huyo wa Ujerumani.

Aliongeza kuwa itakuwa muhimu kabisaa kwamba ushirikishwaji wa kisiasa aliouahidi waziri mkuu Abadi wa Iraq unatekelezwa kivitendo, na watahitaji kuwaendeleza na kuwaimarisha waasi wenye msimamo wa wastani ndani ya Syria, ambao watakuwa katika nafasi ya kuleta uhalali na utawala bora kwa watu wote ndani ya Syria.

Mkutano huo wa kijeshi uliyofanyika kwenye kambi ya jeshi nje ya mji wa Washington, ulikuja baada ya ndege za kivita kufanya mashambulizi 21 katika muda wa siku mbili mjini Kobani. Mashambulizi hayo yalinuwiwa kuwazuwia wapiganaji wa IS ambao wanazidi kusonga mbele mjini humo, na kutishia uwezekano wa mauaji ya watu wengi mbele ya vikosi vya Uturuki na vyombo vya habari vya kimataifa.

Obama alieleza pia wasiwasi juu ya hali inayoendelea katika mkoa wa Anbar nchini Iraq, ambao karibu wote umeangukia mikononi mwa wapiganaji hao, na hivi sasa wako katika kingo za magharibi mwa mji mkuu Baghdad, ambao ndiyo makao makuu ya serikali inayoongozwa na Washia.

Wapiganaji wa Dola ya Kiislamu.
Wapiganaji wa Dola ya Kiislamu.Picha: picture-alliance/abaca/Yaghobzadeh Rafael

Ankara ya yachukuwa tahadhari

Uturuki ambayo imekabiliwa na uasi wa miongo mitatu wa Wakurd, imeimarisha usalama katika mpaka wake na Syria baada ya mapigano mjini Kobani kusababisha wakimbizi wapatao 200,000, lakini inabakia kuwa mshirika mwenye tahadhari.

Wanajeshi wake hawajaingilia mjini Kobani licha ya kuwa mita chache kutoka eneo yanakofanyika mapigano, na bado haijaziruhusu ndege za Marekani kutumia ardhi yake kwa mashambulizi.

Wakurd wanasema hawataki vikosi vya Uturuki ndani ya Kobani, lakini wanaitaka nchi hiyo iruhusu ardhi yake itumike kupitisha zana kwenda kwa Wakurdi wanaoutetea mji wa Kobani, jambo ambalo hadi sasa serikali ya Ankara imelikataa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman