1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yarusha mamia ya droni, makombora kuelekea Israel

14 Aprili 2024

Iran imeanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Israel, ikirusha dazeni kadhaa za droni na makombora kuelekea taifa hilo la Kiyahudi Jumamosi usiku katika hatua iliyotarajiwa pakubwa lakini isiyo kifani katika ukubwa wake.

https://p.dw.com/p/4ejSN
Israeli Ashkeloni | Mfumo wa kuzuia makombora ukifanya kazi baada ya shambulio kutoka Iran
Mfumo wa kuzuia makombora ukifanya kazi baada ya Iran kurusha droni na makombora kuelekea Israeli, kama inavyoonekana kutoka Ashkelon, Israel Aprili 14, 2024.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Mashambulizi hayo yanakuja "kujibu uhalifu wa hivi karibuni wa utawala wa Kizayuni," kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ikimaanisha shambulio linaloaminiwa kufanywa na Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria mwanzoni mwa mwezi huu, ambamo majenerali wawili wa Iran waliuawa.

"Utawala wa uovu utaadhibiwa," alisema kiongozi wa Irani Ayatollah Ali Khamenei katika chapisho la mtandao wa kijamii kwenye jukwaa X, zamani Twitter.

Soma pia: Iran yaikamata meli ya Israel licha ya onyo la Biden

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliandika kwamba "Israel iko imara" katika chapisho kwenye X, mara tu baada ya jeshi la Israel kuthibitisha shambulio la droni la makombora la Iran Jumamosi jioni.

"Taifa la Israel lina nguvu, IDF (Jeshi la Ulinzi la Israel) lina nguvu, watu wa Israeli wana nguvu," Netanyahu aliandika kwenye X, dakika nne tu kabla ya kituo cha jeshi kusema kwamba Iran ilikuwa imerusha ndege zisizo na rubani.

Israeli Jerusalemu | Vitu vilivyo angani baada ya shambulio la Irani
Vitu vikionekana angani juu ya Jerusalem baada ya Iran kurusha droni na makombora kuelekea Israel, mjini Jerusalem Aprili 14, 2024.Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

"Pamoja tutasimama, na kwa msaada wa Mungu - pamoja tutawashinda maadui wetu wote," aliandika.

Katika ujumbe wa video ulioambatana na chapisho lake alisema: "Tuna kanuni iliyo wazi: yeyote atakayetushambulia, tutawamshambulia."

Uadui kati ya Iran na Israel na vita vya Gaza

Israel na Iran zimekuwa mahasimu tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979. Mivutano ya miongo kadhaa kati ya nchi hizo mbili imeongezeka kufuatia kuzuka kwa vita vya Gaza mwezi Oktoba.

Soma pia: Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

Israel imefunga anga lake usiku kujibu shambulio la Iran, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo, vikinukuu mamlaka ya usafiri wa anga. Jordan, Iraq, Lebanon pia ziliripotiwa kufunga anga zao kwa mujibu wa maafisa wa serikali na vyombo vya habari.

"Tunafuatilia kwa karibu ndege za mauaji za Iran ambazo ziko njiani kuelekea Israel," msemaji wa IDF Daniel Hagari alisema. "Hii ni ongezeko kubwa la mivutano na la hatari."

Israeli Jerusalemu | Vitu vilivyo angani baada ya shambulio la Irani
Iran imeishambulia Israel kwa droni na makombora usiku wa Jumamosi, Aprili 13, 2024.Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Alisema uwezo wa Israel wa kujihami na kushambulia uko katika "kiwango cha juu zaidi cha utayarifu kabla ya shambulio hili kubwa kutoka Iran."

Hapo awali, Israeli ilitoa miongozo kwa umma, ikiwashauri kuwa karibu na makazi na kupunguza idadi ya watu ambao wanaweza kukusanyika katika maeneo fulani, kutegemeana na kiwango cha hatari. Shughuli za shule na elimu pia ziliahirishwa kabla ya likizo ya wiki mbili ya Pasaka kuanzia Jumapili.

Israel ilikuwa tayari

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema awali kwamba taifa hilo lilikuwa limejiandaa. "Katika siku za karibuni tumeimarisha mifumo yetu ya ulinzi na mashambulizi na tumedhamiria kuchukuwa hatua zozote zinazohitajika kulinda raia wa taifa la Israel," alisema kwa mujibu wa ofisi yake.

Aliwaambia wananchi kufuata maelekezo yaliyotolewa na jeshi na idara ya usalama wa ndani yaliyotolewa Jumamosi jioni, yalioanza kutumika saa tano usiku na kuendelea kwa kwa saa 48.

Israel Tel Aviv | Baraza la Kivita la Israel na Waziri Mkuu Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akikutana na Baraza lake la kivita katika eneo la Kirya, Tel Aviv, baada ya Iran kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israel.Picha: Israeli Prime Minister Office/AFP

Biden akutana na washauri wake wa usalama

Mjini Washington, Rais Joe Biden alikatisha safari ya wikendi kwenye nyumba yake ya ufukweni mjini Delaware na kurejea Ikulu ya White House. Alitazamiwa kuitisha mkutano wa wakuu wa Baraza la Usalama la Kitaifa siku ya Jumamosi kujadili shambulio hilo, Ikulu ya Marekani ilisema.

Marekani imekuwa mshirika imara zaidi wa Israel na mfadhili wake mkuu wa kijeshi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alilaani "vikali" shambulio la "kizembe" la Iran dhidi ya Israel.

Alisema Uingereza "itaendelea kutetea usalama wa Israel na ule wa washirika wetu wote wa kikanda, ikiwa ni pamoja na Jordan na Iraq." Uingereza na washirika wake walikuwa "wanafanya kazi kwa haraka ili kuleta utulivu," alisema.

Soma pia: Iran yaapa kulipa kisasi dhidi ya walioushambulia ubalozi wake Damascus

Shambulio hilo lilitarajiwa na Marekani na Israel walikuwa wametuma wanajeshi wa ziada katika eneo hilo.

Iran imerusha makombora na droni aina ya Shahed kuelekea Israel.
Iran imerusha makombora na droni aina ya Shahed kuelekea Israel.Picha: Iranian Army Office/ZUMA Wire/IMAGO

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alimhakikishia Gallant "msaada usioyumba wa Marekani" katika mazungumzo ya simu kutokana na "vitisho vikubwa vya kikanda," kulingana na msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pat Ryder.

Austin alisema Israel inaweza "kutegemea msaada kamili wa Marekani" dhidi ya mashambulizi yoyote ya Iran na washirika wake.

Balozi wa Ujerumani nchini Israel, Steffen Seibert, aliwasihi Wajerumani wote walioko nchini Israel, akielezea kile alichokiita "mashambulizi ya moja kwa moja ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo kabla."

Soma pia: Shambulio la Israel Damascus lauwa makamanda wa Iran

Picha zilizosambazwa na shirika la habari la serikali ya Irani IRNA na shirika la habari la Tasnim, ambalo linachukuliwa kuwa chombo cha jeshi la Mapinduzi, zilionyesha makomando wakipiga kelele kutoka kwenye helikopta ya kijeshi hadi kwenye sitaha ya meli. Meli hiyo ilikuwa ikielekea kwenye maji ya Iran baada ya kuzuiliwa, kulingana na IRNA.

Israel yaishutumu Iran kuhusu nyuklia

Ndege za abiria wakati huo huo zilikuwa zinaepuka kupita iran katikati mwa hali ya kitisho cha juu.

Shirika la ndege la Uholanzi, KLM na shirika la Australia la Qantas, yalisema yamefanyia mabadiliko njia za safari zake kuepuka kuruka katika anga hatari.

KLM ilisema ndege zake hazitaruka tena katika anga ya Iran na sehemu kubwa ya Israel kuanzia sasa, kama hatua ya tahadhari," liliripoti shirika la habari la Uholanzi ANP.

Chanzo: dpae, afpe

Mhariri: Daniel Gakuba