Iran kukewa vikwazo na UM keshokutwa ? | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran kukewa vikwazo na UM keshokutwa ?

Iran imepewa muda hadi alhamisi hii kuachana kabisa na mpango wake wa kurutubisha madini ya kinuklia.Mjumbe wa Iran Ali Larijani anakutana leo huko Vienna, na mkuu wa shirika la Atomiki (IAEA) El Baradei.

Mjumbe wa Iran anaehusika na maswali ya nguvu za nuklia Ali Larijani, anakutana hii leo na mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Mohammed El Baradei mjini Vienna,Austria.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipa Iran muda hadi kesho jumatano kusimamisha kurutubisha madini ya uranium ama sivyo ikabiliwe na vikwazo .

Zikisalia siku 2 kabla kumalizika muda wa mwisho iliopewa Iran na UM ,Teheran, yabainika inajaribu kuepusha dhara upande wake.Kwahivyo, mjumbe wake mkuu wa maswali ya nuklia Ali Larijani, aliruka jana kwa safari ya Vienna,Austria.

Leo anakutana huko na Bw.Mohamed El Barradei ambae anatakiwa kulikabidhi wiki hii, Baraza la Usalama la UM ripoti yake juu ya mradi wa Iran.

Lakini, wakati Larijani ambae anapanga pia kukutana na mjumbe wa UU Javier Solana anaashiria utayarifu wa mazungumzo, watawala mjini Teheran, wamekuwa wakisisitiza siku chache zilizopita kubakia na mradi wao wa nguvu za atomiki.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliwazindua wairani mwishoni mwa wiki kuwa akiba ya nishati ya ma futa na gesi ya Iran yaweza ikamalizika .Kwahivyo, wanahitaji kuwa na vinu vya nishati ya kinuklia.Khamenei akasema hivi na ninamnukuklu:

“Mustakbala na hatima ya Iran, haulingani kabisa na mawazo ya nchi za magharibi kuwa Iran eti haihitaji nishati ya kinuklia.” Mwisho wa kumnukulu.

Akaongeza:

“ Wanataka kuwanyima wairani teknolojia ya kinuklia ili Iran ibakie kuwategemea wao na ibakie nyuma.Ni dhahiri-shahiri kuwa, umma wa Iran hautaridhia.”

Kwa matamshi hayo anakariri tena mwanazuoni huyo kile ambacho wiki moja kabla rais wa Iran alinadi siku ya kuadhimisha mapinduzi ya kiislamu ya Iran .Tofauti ni kuwa Mahmoud Ahmadinejad alitumia maneno makali zaidi.

“Ulimwengu mzima tayari unajua kuwa, Iran inafuata msingi wa haki yake isiouzika pamoja na msingi wa sheria za Shirika la Nguvu za Atomiki ulimwenguni.

Na ni haki yetu kwa muujibu wa mapatano ya kimataifa, kuzalisha nishati ya kinuklia.”

Kusema kweli, hakuna kilichobadilika katika Jamhuri ya Kislamu ya Iran tangu pale lilipopitishwa azimio la UM nambari 1737 siku moja kabla siku kuu ya X-masi mwaka jana .

Kwani, Iran, inasisitiza kama hapo kabla ujtayarifu wake wa kuzungumza lakini inaweka wazi kwamba kuzungumza huko kusiambatanishwe na masharti yoyote.Kwa lugha nyengine,Iran haiko tayari kuachana na mradi wake wa nishati ya kinuklia.Kwahivyo, mapema kabisa keshokutwa alhamisi ,vikwazo dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran haviepukiki.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com