IEBC yasema ipo tayari kwa uchaguzi Kenya | Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2017 | DW | 24.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Kenya Yaamua

IEBC yasema ipo tayari kwa uchaguzi Kenya

IEBC yasema iko tayari kwa uchaguzi

Zimesalia wiki mbili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya. Tume huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC, imesema iko tayari kwa zoezi hilo litakalofanyika tarehe 8 Agosti, licha ya changamoto na manung'uniko yanayoiandama kutoka kwa wanasiasa wa mrengo wa upinzani.

Katika kikao na wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi, Tume hiyo huru ya Uchaguzi na Mipaka pamoja na idara ya mahakama kuu zimesema kuwa kila hatua muhimu itachukuliwa kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika  kwa njia nzuri. Dkt Roseline Akombe ambaye ni kamishna katika Tume ya IEBC amesematume hiyo imejiandaa ya kutosha.

Kuhusu suala la kuwaelimisha wapiga kura, Akombe amedokeza kuwa tume inafanya kila iwezalo kutoa mafunzo kwa wapiga kura kote nchini kabla ya siku ya uchaguzi. Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya washika dau kwamba wapiga kura wengi bado hawajapata elimu ya kutosha kuwandaa kwa zoezi la uchaguzi.

Naye Jaji wa mahakama kuu Mbogholi Msagha amesisitiza umuhimu wa idara ya mahakama wakati wa kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi na kuhimiza yeyote aliye na malalamiko kuhusu uchaguzi kuwasilisha kesi katika mahakama. "Ndiyo tuko tayari. Tunaweza kabisa kusema kuwa ndiyo tuko tayari kwa shughuli za uchaguzi. Katiba ya sasa inatuamrisha kwamba mara tu kesi kuhusu malalamishi ya uchaguzi inapowasilishwa kortini basi kesi hiyo isikizwe kunako katika kipindi cha miezi sita peke yake. Na kesi hiyo haiwezi kuongezewa muda."

Aidha Tume ya EBC, inasisitiza kuwa swala la uwajibikaji na uwazi linapewa kipaumbele hasa wakati huu wa kuelekea katika zoezi la uchaguzi mkuu.

Dkt Akombe anatoa mwito kwa Wakenya kudumisha amani na pia kujitokeza kwa wingi wakati wa siku ya kupiga kura.

Uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatajwa kuwa na ushindani mkali ambapo Rais Uhuru Kenyatta anapambana kurudi tena madarakani dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga.

Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com