1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yakosoa mkopo wa Benki ya Dunia kwa Tanzania

3 Aprili 2020

Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema Benki ya Dunia imeidhinisha mkopo kwa Tanzania bila kuilazimisha nchi hiyo kukomesha sera yake ya kuwakufuza shule wanafunzi wa kike waliopata ujauzito.

https://p.dw.com/p/3aOTr
Tansania Schülerinnen
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kupitia taarifa yake iliyotolewa siku moja tangu benki ya dunia ilipopiga kura kuidhinisha mkopo huo kwa Tanzania, shirika la Human Rights Watch limesema chombo hicho cha kimataifa kimeshindwa kutumia nafasi iliyokuwepo kuishinikiza serikali ya Tanzania kuachana na sera za kibaguzi na zinazowakandamiza wengine.

Mtafiti mwandamizi wa Human Rights Watch Elin Martinez ameonya kuwa uamuzi huo umetia doa msimamo wa jadi wa benki ya dunia wa kupinga ubaguzi na kuhimiza mifumo ya haki inayotoa nafasi kwa makundi yote ndani ya jamii.

Mnamo Machi 31 benki ya dunia iliridhia kuipatia Tanzania mkopo wa kiasi dola milioni 500 ambao ni sawa na shilingi za Tanzania Trilioni moja kufadhili mpango wa kuboresha elimu ya sekondari.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuahirishwa kwa miezi kadhaa kufuatia wito wa mashirika yasiyo ya serikali na wanasiasa wa upinzani waliotaka Tanzania isipatiwe mkopo huo hadi itakaporekebisha msimamo wake unaowazuia wanafunzi wa kike waliopata mimba kurejea shule.

Hata hivyo Benki ya Dunia imearifiwa kuwa benki ya dunia imetoa mkopo huo kwa Tanzania bila kuzingatia wasiwasi ulioelezwa na makundi ya haki za kiraia.

Msimamo wa rais Magufuli kuhusu mimba kwa wanafunzi 

Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Rais John Magufuli amesisitiza mara kadhaa kuwa wanafunzi waliopata mimba hawatorejea  kwenye mfumo rasmi wa elimu wakati wote muhula wa utawala wake.

Wakosoaji wake wamesema msimamo huo unawanyima haki ya elimu maelfu ya wanafunzi wa kike wanaolazimishwa kukatiza masomo na kutorejea shuleni hata baada ya kujifungua.

Inakadiriwa kiasi wanafunzi 5,500 wanaopata ujauzito wanakatiza masomo kila mwaka katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Kadhalika watetezi wa haki za binadamu wamesema kuwa sera hiyo inawalazimisha wanafunzi wa kike kufanyiwa vipimo vya ujauzito kwa lazima na kuwakufuza shule moja kwa moja wote waliobeba mimba.

Kulingana na Human Rights Watch mkopo uliotolewa kwa Tanzania unajumuisha  fedha za kutayarisha mfumo mbadala wa elimu utakaotumiwa na wanafunzi walioacha masomo katika utaratibu rasmi.

Mfumo mbadala wapingwa na wanaharakati 

Tansania Kondora Mädchenschule
Picha: DW/N. Quarmyne

Mfumo huo unapigiwa upatu na serikali ya Tanzania kuwa njia pekee ya kuwasaidia watoto walioshindwa kumaliza masomo ikiwemo wale waliopata ujauzito.

Hata hivyo mfumo huo unapingwa na watetezi wa Haki za Binadamu wakisema utaanzisha vituo  vya malipo kwa wanafunzi watakaojiunga na hautatoa mtaala kamili kwa wanafunzi kaam ilivyo katika mfumo rasmi wa elimu.

Kupitia taarifa yake Human Rights Watch imeitaka benki ya dunia kutotoa awamu ya kwanza ya fedha za mkopo huo hadi serikali ya Tanzania itakapoheshimu wajibu wake wa kutoa elimu sawa na kwa wote ikiwemo wasichana.

Shirika hilo limerejea msimamo wake wa kuinishikza serikali ya raia Magufuli kuachana na sera yake kuhusu ujauzito na kuwafukuza shule wanafunzi wa kike.

Mwandishi: Rashid Chilumba /https://www.hrw.org/news/2020/04/02/tanzania-world-bank-okays-discriminatory-education-loan

Mhariri: Josephat Charo