1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkopo wa Tanzania unapaswa kukuza elimu ya wasichana wote

Grace Kabogo
24 Aprili 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limesema Benki ya Dunia inapaswa kushirikiana na Tanzania kuhakikisha wasichana wote wajawazito na wanafunzi wenye watoto wanaendelea na masomo kwenye shule za umma. 

https://p.dw.com/p/3bLlc
Tansania Schülerinnen
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Katika ripoti yake iliyotolewa siku ya Ijumaa, shirika hilo la Human Rights Watch imesema Benki ya Dunia haipaswi kulipa deni la awali la mkopo wa elimu la 1990 kwa Tanzania ambalo limepangwa kutolewa 2021, hadi hapo serikali hiyo itakapohakikisha kwamba wasichana wote wanapata elimu sawa katika shule za msingi na sekondari.

Machi 31, Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa Dola milioni 550 kwa Tanzania kwa ajili ya mpango wa elimu ya sekondari. 

Kwa kufanya hivyo, Benki ya Dunia ilipuuza sera ya serikali iliyoungwa mkono na Rais John Magufuli ambayo inawazuia wanafunzi wanaopata mimba na wanafunzi wenye watoto kuendelea na masomo kwenye shule za serikali.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, Benki ya Dunia imetoa taarifa isiyo sahihi ambayo inakanusha uwepo wa sera hiyo na kupuuza matokeo ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yameelezea athari zake. 

Menschenrechte Logo human rights watch
Nembo ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, HRW

Mtafiti Mkuu wa haki za wanawake katika shirika la Human Rights Watch, Agnes Odhiambo, amesema Benki ya Dunia ambayo ndiyo mfadhili mkuu wa Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kusaidia kuhakikisha kila msichana nchini Tanzania anapata elimu bila ya kubaguliwa.

Odhiambo amesema Benki ya Dunia inapaswa kuhakikisha kwamba uwekezaji wake unaimarisha na sio kudhoofisha haki za binaadamu kwa wasichana wote wa Tanzania.

Mkopo wa Benki ya Dunia wazusha maswali

Ripoti ya Human Rights Watch imesema katika kuidhinisha mkopo huo, Benki ya Dunia haikuzungumzia wasiwasi juu ya marufuku hiyo, hali inayozusha maswali mengi kuhusu uwajibikaji wake katika kuitokomeza sera hiyo. 

Aprili 6, wizara ya elimu, sayansi na teknolojia ya Tanzania ilitoa taarifa kuhusu mkopo wa Benki ya Dunia, ikisema kwamba Mpango wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari nchini humo, SEQUIP, utafanyika bila ubaguzi na utawajumuisha wasichana ambao waliacha masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito. Hata hivyo, wizara haikufafanua iwapo wasichana wanaopata mimba wataweza kuendelea na masomo kwenye shule za kawaida za serikali.

Shirika hilo limesema serikali ya Tanzania inapaswa kuondoa mara moja marufuku hiyo na kuizingatia sera ya haki za binaadamu ya kuwasaidia wanafunzi wote wajawazito kuendelea na masomo. Odhiambo anasema kwa kuidhinisha mkopo huo, Benki ya Dunia imepitisha hatua zisizofaa, kama vile elimu duni, ambazo zinawabagua wasichana na kuunga mkono sera kandamizi za serikali.


(HRW)