Hong Kong yapiga marufuku biashara ya pembe za ndovu | Masuala ya Jamii | DW | 06.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Hong Kong yapiga marufuku biashara ya pembe za ndovu

Wabunge wa Hong Kong wameidhinisha pendekezo la serikali la kupiga marufuku mauzo ya bidhaa zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu nchini China ifikapo mwaka 2021.

Wabunge wameiunga mkono hatua hiyo kwa kupiga kura 49 dhidi ya kura 4 kutaka kubadilisha sheria iliyopo kwa sasa, ya kupiga marufuku mauzo ya bidhaa zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu Hong Kong ambapo watafiti wanasema eneo hilo ndilo eneo kubwa la soko ya bidhaa hizo.

Pendelezo lililotolewa na serikali linajumuisha pia adhabu kali kwa watakaoendelea kufanya ujangili wa ndovu na wanyama wengine walio katika hatari ya kutoweka.  Chini ya sheria hiyo mpya faini itakayotolewa kwa wavunja sheria imeongezeka mara mbili na kufikia dola milioni 1.3 au kifungo cha miaka 10 jela, kifungo kilichoongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo zamani cha miaka miwili.

Sheria hiyo mpya itaanza kufanya kazi hatua kwa hatua huku marufuku kamili ikitekelezwa mwishoni mwa mwaka 2021 ambapo muda wa leseni ya wanaofanya biashara hiyo utamalizika. Kwa upande wao, Wanaharakati wa kutetea haki za wanyama pori wameisifu hatua hiyo licha ya Hong Kong kuchukua hatua za pole pole zaidi kuliko China bara katika kutekeleza marufuku hiyo.

China ambayo ni muingizaji mkubwa wa bidhaa za pembe za ndovu duniani ilipiga marufuku uuzwaji wa bidhaa hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya kufunga viwanda vyote vinavyotengeneza bidhaa hiyo pamoja na maduka Mwezi machi mwaka jana.

"Kupigwa marufuku bidhaa ya pembe za ndovu na kuwepo adhabu kali mjini Hong Kong, inaonyesha kujitolea kulinda maisha ya baadaye ya tembo wa Afrika, hii itasaidia kupunguza ujangili wa wanyama pori na biashara haramu ya pembe za ndovu ," alisema Cheryl Lo wa shirika la mfuko wa wanyamapori duniani la world wildlife fund.

Sheria iliyoko Hong Kong iliruhusu uuzaji wa bidhaa zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu kabla ya uwepo wa mkataba wa biashara ya kimataifa ya wanyama walio katika hatari ya kupotea,  CITIES chini ya mkataba huo bishara hiyo ilianza kudhibitiwa katikati yam waka 1970 kabla ya marufuku kuwekwa mwaka 1990 katika mauzo ya kimataifa.

Kwa upande mwengine mashirika ya kutetea haki ya wanyamapori yametoa wito kwa mataifa mengine ya bara Asia kama vile Vietnam, Laos, Cambodia na Japan pia kupiga marufuku biashara ya bidhaa za pembe za ndovu, yakisema kuna ushahidi kwamba masoko kama hayo yanaendelea kuwahudumia wageni kutoka China.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com