Hisia kutoka Tanzania kuhusu uchaguzi wa Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 07.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Hisia kutoka Tanzania kuhusu uchaguzi wa Kenya

Wengi wanaojadili uchaguzi huo wanaufananisha na uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2015, ambao pia ulitawaliwa na ushindani usiopata kushuhudiwa. Baadhi ya wanasiasa Tanzania wametangaza wanaegemea upande upi wanaunga mkono.

Uchaguzi wa Kenya ni moja ya mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika eneo la Afrika Mashariki ikiwamo huko nchini Tanzania ambako miaka mitatu iliyopita ilikuwa na uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa kama huu wa sasa wa Kenya. Baadhi ya wanasiasa wa Tanzania wamekuwa wakitajwa mara kwa mara katika uchaguzi huo wa Kenya.

Kauli za Watanzania

Licha kwamba uchaguzi huo unabeba hatma ya Kenya, lakini wananchi wa Tanzania na wanasiasa wake hawajajiweka kando kuuzungumzia na baadhi wakidiriki kuweka ubashiri wao kuhusu wagombea wote wawili.

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa

Maoni mengi ya wananchi ni kuhusu nafasi ya wananchi wa Kenya kutumia kura yao vyema ili kuliepusha taifa hilo na machafuko yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007, machafuko ambayo yalisababisha baadhi ya wananchi kukimbilia katika nchi jirani.

Wengi wanaojadili uchaguzi huo wanaufananisha na uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2015, ambao licha ya kutawaliwa na ushindani usiopata kushuhudiwa, lakini ulimalizika kwa amani na utulivu, hivyo wanawataka Wakenya kuiga mfano huo.

Upinzani Tanzania waunga mkono Uhuru?

Wanasiasa wa Tanzania wamekuwa wakitajwa mara kwa mara katika uchaguzi wa mwaka huu kwa Kenya, hatua ambayo imezidi kuufanya uchaguzi huo kuwa wa vuta nikuvute. Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania na mgombea urais wa muungano wa upinzani katika uchaguzi uliopita, Edward Lowassa, ameweka hadharani turufu yake akimuunga mkono mgombea wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta.

Ingawa hatua yake hiyo ilikosolewa vikali na kambi ya NASA inayoongozwa na mgombea wake, Raila Odinga, lakini Lowassa mbali ya kusisitiza uungwaji wake mkono kwa Jubilee amewasihi Wakenya kuzingatia amani.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Kwa upande mwengine, mara kadhaa serikali ya Tanzania imekuwa ikitajwatajwa kwenye uchaguzi huo madai hayo yamepuuzwa vikali na Waziri wa Mambo ya Nje, Agustine Mahige aliyesema kuwa Tanzania haijachukua upande wowote juu ya uchaguzi huo.

Urafiki wa Magufuli na Raila

Hata hivyo, Rais John Magufuli na Raila Odinga ni marafiki wa karibu hata kabla ya Magufuli kuwa rais. Urafiki wao huo ulidhirika zaidi hivi karibuni wakati Rais Magufuli alipomwalika Odinga nyumbani kwake huko Chato.

Hilo ingawa halimaanishi moja kwa moja kwamba Rais Magufuli anamuunga mkono Odinga kwenye uchaguzi, lakini wafuatiliaji wa mambo wanasema kwa vyovyote vile rafiki angelimpendelea mema rafikiye.

Wakati raia wa Kenya kesho watashuka kwenye vituo vya kupiga kura, wananchi wa taifa hilo walioko katika nchi za Afrika Mashariki nao watajitokeza katika ofisi za ubalozi kupiga kura zao.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Moahmmed Khelef

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com