Hariri asema yuko tayari kurudi Lebanon | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hariri asema yuko tayari kurudi Lebanon

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri amesema yuko huru nchini Saudi Arabia na kwamba atarudi Lebanon hivi karibuni.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri ambaye tangazo lake wiki iliyopita kupitia kituo cha televisheni akiwa Saudi Arabia kuwa amejiuzulu lilisababisha mshtuko katika kanda hiyo ya Mashariki ya kati amesema yuko huru nchini Saudi Arabia na kwamba atarudi Lebanon hivi karibuni.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni mjini Riyadh, Hariri aliyapuuza mbali madai kuwa amewekwa katika kifungo cha nyumbani nchini Saudi Arabia, badala yake alitangaza kuwa atarudi Mjini Beirut-Lebanon  mnamo siku mbili au tatu zijazo.

Wakati wa mahojiano hayo, Hariri aliyeonekana mchovu, alizungumza polepole lakini kwa ukakamavu.

"Nitarudi Lebanon hivi karibuni na nitafuata taratibu za kujiuzulu. Mtanipa muda niweze kujipa usalama ndani ya Lebanon, sizungumzi kuhusu wiki wala miezi bali ninazungumza kuhusu siku chache na haya yametatuliwa."

Mnamo tarehe 4 mwezi huu, Hariri mwenye umri wa miaka 47, alitangaza kupitia kituo cha televisheni akiwa mjini Riyadh kuwa amejiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu wa Lebanon, na tangu wakati huo, hajarejea nchini Lebanon.

Rais Miche Aoun hajakubali rasmi kujiuzulu kwa al-Hariri

Rais wa Lebanon Michel Aoun na Saad al-Hariri wakiwa Baabda (18.12.2016)

Rais wa Lebanon Michel Aoun na Saad al-Hariri wakiwa Baabda (18.12.2016)

Hata hivyo, rais wa Lebanon Michel Aoun hajakubali rasmi kujiuzulu kwa waziri huyo mkuu akisema nyendo zakezimezuiliwa na kudhibitiwa.

Hariri ambaye pia ana uraia wa Saudi Arabia aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye mwenyewe ndiye aliyeiandika barua ya kujiuzulu na amekuwa akitaka kuiwasilisha Lebanon ila kuna hatari.

Alionekana pia kuwa tayari kuibatilisha hatua yake ya kujiuzulu ikiwa machafuko katika kanda hiyo yatasitishwa.

"Kinachofanyika katika kanda yetu ni kitisho dhidi ya Lebanon haswa tunapojiweka katika nafasi zinazoiweka nchi kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi. Tayari tunajua vikwazo vya Marekani, lakini kuongezea tena vikwazo vya nchi za Kiarabu, hatuna haja na hilo."

Kujiuzulu ghafla kwa Hariri kulitokea wakati kukiwa na mvutano ikati ya Saudi Arabia na Iran ambazo zinaunga mkono upinzani katika mivutano ya kuwania mamlaka kuanzia Lebanon, Syria hadi Yemen.

Msanii wa Lebanon akichora picha ya Waziri Mkuu wa Lebanon al-Hariri mjini Beirut

Msanii wa Lebanon akichora picha ya Waziri Mkuu wa Lebanon al-Hariri mjini Beirut

Iran yakana kuingilia mambo ya ndani ya Lebanon

Iran imesema kuwa haiingilii mambo ya ndani ya Lebanon. Hariri aliilaumu Iran na washirika wake nchini  Lebanon  Hezbollah kwa kuiteka nchi yake na kuuyumbisha udhibiti wa mipaka ya kanda hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa UfaransaJean-Yves Le Drian ametoa wito kutaka nchi yoyote isiingilie mambo ya ndani ya Lebanon na pia kuwawezesha viongozi wakisasa kusafiri kwa uhuru na kutoa nafasi ya kupatikana suluhisho la kisasa.

Huku wasiwasi ukizidi, kwa mujibu wa ripoti ambayo wanadiplomasia wamelionesha shirika la ahabari la AFP, Jumuiya ya kiarabu imesema itafanya mkutano maalum Jumapili ijayo kufuatia ombi la Saudi Arabia kujadili ukiukaji unaofanywa na Iran katika kanda hiyo.

Mnamo Wiki iliyopita, hariri alifanya misururu ya mikutano na wanadiplomasia na maafisa wa Saudi Arabia mjini Riyadh akiwemo mfalme Salman .

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com