1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali shuwari katika bustani ya Taksim

12 Juni 2013

Polisi ya Uturuki imefanikiwa kurejesha hali ya utulivu katika bustani yaTaksim,kitovu cha maandamano ya siku 12 dhidi ya serikali.Waziri mkuu Erdogan atakutana na wawakilishi wa baadhi ya makundi ya waandamanaji.

https://p.dw.com/p/18oAZ
Kijana aliyevaa barakoa amenyanyua upanga wa mbao nyuma ya kizuwizi kilichowekwa katika bustani ya Gezi mjini IstanbulPicha: Reuters

Tangu alfajiri bustani ya Taksim iliokuwa imejaa takataka na mabaki ya vizuwizi vilivyosagwa sagwa na vifaru vya kijeshi,ilikuwa tupu na taxi zikaruhusiwa kwa mara ya kwanza katika bustani hiyo.Mamia ya waandamanaji lakini bado wamepiga kambi katika bustani ya karibu na hapo Gezi.

Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan amekubali kukutana na baadhi ya wawakilishi wa waandamanaji wanaowaleta pamoja wafuasi wa makundi yanayopinga kujumuishwa dini katika shughuli za serikali,makundi ya siasa kali za mrengo wa shoto,waliberali,walinzi wa mazingira na wanafunzi.

Jukwaa la mshikamano wa Taksim,kudi mojawapo kati ya waasisi wa vuguvugu hilo linasema wawakilishi wake hawajaalikwa katika mazungumzo hayo na kusisitiza pia hawataki kushiriki kwa wakati wote ambao matumizi ya nguvu yanaendelea.

"Tutaendelea na operesheni zetu bila ya kuchoka,naiwe usiku au mchana hadi wabishi wote watakapotimuliwa katika bustani ya umma"ameonya gavana wa Istanbul Huseyin Avni Mutlu kupitia televisheni ya taifa.

Vikosi vya usalama vimeingilia kati pia mjini Ankara,mji mkuu wa Uturuki kuwatimua waandamanaji.

Marekani yahimiza mazungumzo

Türkei Premierminister Recep Tayyip Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: imago/Xinhua

Maafisa wa serikali wanasema hawatowaandama "waandamanaji halali" wanaopiga kambi katika bustani ya Gezi wakilalamika dhidi ya mipango ya serikali ya kujenga majumba makubwa makubwa katika bustani hiyo.

Akijinata kwa kushinda mara tatu katika uchaguzi mkuu : mwaka 2002,2007 na 2011 waziri mkuu Erdogan,mhafidhina anasemekana kuelemea zaidi upande wa kidini na ambae waandamanaji wanakosoa mtindo wake wa uongozi,anasema maandamano hayo yanachochewa na wafanyafujo,magaidi na makundi kutoka nje.

Machafuko hayo yanachafua hadhi ya Uturuki kama dola la kidemokrasia na soko huru ,hadhi inayoenezwa ulimwenguni na chama cha waziri mkuu- AKP tangu zaidi ya mmongo mmoja uliopita.Soko la hisa la mjini Istanbul limepoteza zaidi ya asili mia 11 tangu maandamano yalipoanza.

Marekani imeelezea wasai wasi wake kuhusu kitisho cha kukabwa uhuru wa mtu kutoa maoni yake na kutoa wito wa mazungumzo kati ya serikali na waandamanaji.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman