1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jengo la makumbusho nchini Uturuki kugeuzwa msikiti

Saleh Mwanamilongo
2 Julai 2020

Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan anataka kuwavutia wapiga kura kwa kuligeuza eneo maarufu la kitalii la Hagia Sophia kuwa msikiti.

https://p.dw.com/p/3ei9Z
Jengo la makumbusho la Hagia Sophia mjini Instabul
Jengo la makumbusho la Hagia Sophia mjini Instabul Picha: picture-alliance/akg/Bildarchiv Steffens

Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan anataka kuwavutia wapiga kura kwa kuligeuza eneo maarufu la kitalii la Hagia Sophia kuwa msikiti. Lakini mpango wake huo unakabiliwa na upinzani mkali. Hagia Sophia lilikuwa kanisa kuu la madhehebu ya Orthodox enzi za utawala wa Byzantine ambalo lilibadilishwa kuwa msikiti baada ya kutekwa kwa mji wa Constantinapoli, lakini baadaye likawa jengo la makumbusho kwa watu wa imani zote katika Uturuki ya enzi za mpya.

Hagia Sophia ndio alama kubwa ya mji wa Instabul, ambao kama Constantinapoli ulikuwa mji mkuu wa enzi ya Wakristo wa Byzantine hadi pale Ottoman ambaye alikuwa Muislamu alipouteka mji huo mwaka 1453.

Kila mwaka mamilioni ya watalii wanalitembelea eneo hilo hasa kutokana na ubora wa usanifu majengo yake, uliosababisha jengo hilo kuwa miongoni mwa maeneo yanayohifadhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamadni, UNESCO. Kanisa la Hagia Sophia, lililojengwa karne ya sita na kufanywa msikiti katika mwaka 1453 na hatimae katika mwaka 1935 kuwa jumba la makumbusho linalovutia watalii kutoka kila pembe ya dunia.

Hatua ya kisiasa ya chama cha AKP

Jengo la makumbusho la Hagia Sophia mjini Instabul, Uturuki
Jengo la makumbusho la Hagia Sophia mjini Instabul, UturukiPicha: Getty Images

Hivi sasa rais Recep Tayyip Erdogan anataka kuligeuza jengo hilo, lililoko kwenye wilaya ya Fatih, katikati ya Instabul kuwa msikiti kwa ajili ya mamilioni ya wapiga kura, wengi wao wakiwa na mafungamano ya kidini. Kwao Hagia Sophiani ni alama ya ushindi wa Waislamu enzi za utawala wa Ottoman dhidi ya Wakristo wa enzi za utawala wa Constantinopoli.

Erdogan ambae pia ni mwenyekiti wa chama tawala cha Haki na Maendeleo, AKP anatarajia kugeuza hatua ya muanzilishi wa taifa la Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk kwa kuigeuza Hagia-Sophia kuwa msikiti. Kwa muda mrefu nchini Uturuki hatua hiyo imekuwa ikijadiliwa lakini Alhamisi, baraza la Kitaifa, moja wapo ya mahakama ya juu ya Uturuki ilielezea kwamba inachunguza uhalali wa amri ya rais wa zamani Ataturk ya mwaka 1935 ya kugeuza Hagia Sophia kuwa eneo la makumbusho.

Umazi wa mahakama unatarajiwa kutolewa mnamo kipindi cha siku 15. Hatua ya chama cha AKP inafuatiwa na misimamo ya kizalendo. ''Hagia Sophia ni eneo letu la kijiografia. Wale walioutegega mji huu kwa nguvu ya silaha wana haki pia ya kuudhibiti. Hagia Sophia iko chini ya mamlaka yetu,'' alisema  naibu mwenyekiti wa chama tawala cha AKP, Numan Kurtulmus.

Siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 567 ya ushindi wa Constantinapoli, chama cha AKP kiliruhusu moja wapo wa ma imamu kwenda kusoma maandishi ya kur'ani kwenye eneo la Hagia Sophia.