1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utoaji kibali cha Kombe la Dunia 2026 wacheleweshwa

10 Juni 2015

Shirikisho la Kandanda Duniani, FIFA, ambalo linakabiliwa na kashfa kubwa ya rushwa, limeahirisha leo mchakato wa utoaji kibali cha kuandaa dimba la Kombe la Dunia la mwaka wa 2026

https://p.dw.com/p/1FekQ
Fußball WM 2014 Finale Argentinien Deutschland
Picha: Reuters

Badala yake, shirikisho hilo limeanza shughuli ya kumtafuta mrithi wa rais wake anayeondoka, Sepp Blatter.

Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, amesema kuwa litakuwa "jambo lisilo maana" kuanza mchakato wa kutoa kibali hicho kwa wakati huu. Wakati huo huo, FIFA imesema kuwa kamati yake kuu itaandaa mkutano maalum mwezi Julai ili kujadili kuhusu "mapendekezo kadhaa" ya tarehe za kuandaliwa mkutano wa baraza kuu utakaomchagua atakayechukua nafasi ya Blatter.

Kura ya kuitafuta nchi itakayoandaa kombe la dunia mwaka 2026 inatarajiwa kufanyika mjini Kuala Lumpur mwezi Mei mwaka 2017.

Marekani iko kifua mbele kuandaa michuano hiyo lakini Canada, Mexico na Colombia pia zimewasilisha maombi ya kutaka kuwa wenyeji wa tamasha hilo

Urusi na Qatar zilichaguliwa kuandaa michuano ya mwaka 2018 na 2022 kupitia kura ya siri iliopigwa na wanachama wakuu wa FIFA wapatao 22 mnamo mwezi Disemba mwaka 2010. Lakini viongozi wa mashtaka nchini Uswizi wanachunguza madai ya ufisadi yanayozunguka zabuni hizo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef