1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola yashuka, Euro yapanda

Maja Dreyer24 Septemba 2007

Thamani ya sarafu ya Dola ya Kimarekani inazidi kupungua na ile ya EURO inaongezeka ikilinganishwa na Dola. Ni jambo ambalo linasababisha athari na faida kwenye pande zote mbili.

https://p.dw.com/p/CHjE
Sarafu moja ya Euro ina thamani kubwa kuliko noti ya Dola moja
Sarafu moja ya Euro ina thamani kubwa kuliko noti ya Dola mojaPicha: AP

Kwa mara ya kwanza thamani ya sarafu ya Euro imezidi Dola 1 na senti 40 za Kimarekani. Sababu yake hasa ni upungufu wa kiwango cha riba Marekani wiki iliyopita. Tokeo lake ni kwamba sarafu ya Dola haivutii sana na wengi wanauza EURO badala ya Dola. Kulingana na wataalamu wa kiuchumi thamani ya Dola inaweza kupungua na ile ya EURO kupanda hadi kuwa EURO moja kua Dola 1 na senti 45 ya Dola za Kimarekani.

Kwa upande wa nchi za Umoja wa Ulaya, maana yake ni kwamba makampuni yanayouza bidhaa zao nje yatapata shida kwa vile iwapo thamani ya sarafu inapanda, bei ya bidhaa pia inapanda. Waziri wa masuala ya uchumi wa Ujeruman, Bw. Michael Glos alionya kuwa ikiwa thamani ya Dola inazidi kupungua, biashara nchini humu itaathirika.

Hayo aliyathibitisha Martin Hüfner, mshauri katika masuala ya bishara: “Tukifika kiwango cha Dola 1 senti 45 kwa Euro moja inaanza kuwa ni vigumu kwa baadhi ya makampuni. Nadhani tukishafika kiasi cha 1 na senti 50 inabidi kuchukua hatua ya kuzuia athari zaidi. Yaani gharama kwa makampuni zinazidi. Na pia bajeti inayobakia kulipa mishahara inapungua.”

Kwa sasa, mtaalamu Bw. Hüfner haoni sababu ya kuwa na wasiwasi hususan nchini Ujerumani ambayo ni nchi ya Ulaya inayouza zaidi nje. Uchumi wa Ujerumani umejiandaa vizuri kwa kiasi kikubwa cha thamani ya Euro alisema Bw. Hüfner. Lakini sarafu ngumu ya EURO pia ina faida fulani kwa mataifa ya Ulaya, hususan kuhusiana na bei ya mafuta yanayoingizwa kutoka nje. Bei yake itakuwa ndogo kulingana na EURO kwa sababu mafuta yanauzwa kwa Dola. Vilevile bidhaa nyingine zinazonunuliwa nje zitakuwa rahisi zaidi wa nchi za Ulaya.

Kwenye upande mwingine wa bahari ya Atlantiki, huko Marekani, ni kinyume chake. Bei za bidhaa zinazonunuliwa nje zinapanda na mauzo ya nje yatakuwa rahisi zaidi na hivyo kuongeza nafasi kwa uchumi wa Marekani. Hata hivyo, upungufu wa thamani ya Dola unaongeza hatari kwa wale wanaonunua hati za kiserikali ambazo zinatumika kulipa madeni ya umma. Kwa mara ya kwanza tangu muda wa miaka 31 iliyopita thamana ya Dola ya Kimarekani ni sawa na Dola ya Canada.

Benki kuu ya Marekani iko katika hali ngumu. Wiki iliyopita ilichukua hatua ya kushtua kwa kupunguza riba kwa asilimia 0.5 hadi asimilia 4.75. Wataalamu kadhaa walitoa hoja kwamba kwa kupungua riba, masoko ambayo yamekwama, yanafungua na mahitaji ya Dola yataongezeka. Walitarajia kuwa bei ya dhahabu itapungua na thamani ya Dola itaongezeka. Hiyo lakini haikutokea.

Matatizo ya sarafu ya Dola pia yanazitia wasiwasi nchi za Kiarabu ambazo zinauza mafuta. Nchi kadhaa ikiwemo Saudi Arabia zinafikiria upya kutoweka tena kima cha sarafu yao sawa na Dola ya Kimarekani. Tayari nchi hizo nyingi zinakabiliwa na tatizo la kupanda kwa bei za bidhaa. Kuna hofu kwamba hatua hiyo itasababisha mauzo ya kiwango cha juu ya Dola duniani na kuiongezea matatizo sarafu ya Dola. China pia imenunua kiasi kikubwa cha Dola kama akiba. Mara kwa mara inatishia kuuza Dola zake na hivyo kuishinikiza serikali ya Marekani.