Cyril Ramaphosa achaguliwa kuwa rais mpya wa Afrika Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 15.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Afrika Kusini

Cyril Ramaphosa achaguliwa kuwa rais mpya wa Afrika Kusini

Chama cha ANC nchini Afrika Kusini kimemteua Cyril Ramaphosa kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Hayo ni baada ya uongozi wa miaka tisa wa Jacob Zuma kumalizika kutokan na shinikizo la kumtaka aachie madaraka

Kwanza mwanasheria mkuu wa Afrika Kusini aliusoma waraka wa kujiuzulu rais Jacob Zuma na kuhakikisha kuwa waraka huo umetiwa saini na kiongozi huyo wa zamani. Wakati hayo yakiendelea wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) walitoka bungeni wakisema uchaguzi huo wa chama cha ANC haukuwa halali.

Chama hicho cha upinzani kinachoongozwa na Julius Malema, awali kilikuwa kimesema hakitashiriki katika uchaguzi huo bungeni wa kumteua rais mpya kwa sababu chama tawala cha ANC kimejawa na kashfa za rushwa. Malema amesema badala yake bora bunge lingevunjwa na kisha kupisha nafasi ya kuchaguliwa wabunge wapya kwenye uchaguzi wa mapema.

Kushoto: Jacob Zuma rais aliyejiuzulu. Kulia: Rais mpya wa Afrika Kusini Cyril Ramaposa(Reuters/S. Sibeko)

Kushoto: Jacob Zuma rais aliyejiuzulu. Kulia: Rais mpya wa Afrika Kusini Cyril Ramaposa

Bunge la Afrika Kusini lenye wawakilishi wapatao 400 wengi kutoka chama tawala cha ANC ndio wamemchagua bwana Cyril Ramaphosa kumrithi Jacob Zuma, ambaye alijiuzulu kutoka kwenye wadhfa huo wa Rais hapo jana siku ya Jumatano. Ramaphosa amechaguliwa bila kupingwa kwani alikuwa ni mgombea pekee asiye na mpinzani, mwanasheria mkuu bwana Mogoeng Mogoeng aliwaambia wabunge waliokusanyika bungeni.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini Julius Malema (picture-alliance/dpa/C. Tukiri)

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini Julius Malema

Kiongozi wa upinzani Julius Malema amesema chama tawala cha ANC kilimlinda Jacob Zuma kwa miaka kadhaa iliyotawaliwa na rushwa na hivyo haoni iwapo chama hicho kitabadili mwenendo wake chini ya uongozi wa Ramaphosa ijapokuwa ameahidi kupambana na rushwa.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) nchini Afrika Kusini Mmusi Maimane (picture-alliance/AP Photo/H. Verwey)

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) nchini Afrika Kusini Mmusi Maimane

Kiongozi wa chama kingine cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) Mmusi Maimane amemuunga mkono bwana Malema kwa kusema, huo ni mtazamo wa pamoja kwamba chama cha ANC kimekuwa kinakiuka katiba, na kulinda uhalifu. Kwa hiyo wanataka kutafakari kifungu cha 50 cha katiba ambacho kinashurutisha bunge livunjwe na kusisitiza kwamba yeyote anayetaka kuiongoza nchi hiyo, basi ni lazima awe na ridhaa kutoka kwa watu wa Afrika Kusini.

Viongozi hao wa vyama viwili vikuu vya upinzani nchini Afrika Kusini vya Economic Freedom Fighters, EFF na Democratic Alliance, DA mnamo tarehe 12 mwezi huu wa Februari walitoa tamko la kutaka bunge livunjwe na kisha uchaguzi mpya ufanyike wakati ambapo masaibu yaliyokuwa yanamwandama rais Jacob Zuma yalipozidi hadi hapo jana alipojiuzulu.

Cyril Ramaphosa aliyeanzia katika mji wa Soweto hadi kuwa kiongozi, mwanaharakati wa kupambana na ubaguzi wa rangi na pia mfanyabiashara tajiri leo hii Alhamisi amechaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo amesema ameupokea wadhfa huo kwa unyenyekevu na yuko tayari kuwatumikia watu wa Afrika Kusini.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/RTRE/DPA

Mhariri:Josephat Charo