1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba yakasirishwa na kauli za vitisho za Trump

18 Machi 2026

Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel amemjibu rais Donald Trump kuhusu matamshi yake yaliyoashiria kwamba kuna uwezekano wa Marekani kuitwaa Cuba.

https://p.dw.com/p/5AbSu
Rais wa Cuba  Díaz-Canel aionya Marekani, Cuba haitokubali kuyumbishwa
Rais wa Cuba Díaz-Canel aionya Marekani, Cuba haitokubali kuyumbishwaPicha: Norlys Perez/REUTERS

Rais Diaz wa Cuba,amesema Marekani itakabiliwa na upinzani mkubwa kabisa usioyumba ikiwa itajaribu kulichukuwa taifa hilo la kisiwa ambalo kwa sasa linakabiliwa na hali ya mbaya ya umasikini,ambayo watawala wake wanahangaika kujaribu kuidhibiti, kutatuwa matatizo ya ukosefu wa umeme yanayoshuhudiwa nchi nzima.

Siku ya Jumatatu wiki hii rais Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba anaamini upo uwezekano wa kuichukuwa Cuba na atakapofanya hivyo hilo litakuwa jambo zuri.

Aliyasema hayo akiwa ndani ya Ikulu ya WhiteHouse wakati wa kusaini sheria kadhaa za kiutendaji nchini Marekani.Katika ujumbe wake kwenye ukurasa wa X kiongozi wa Cuba Diaz-Canel ametowa Ujumbe kwa Marekani akisema Washington imekuwa ikitowa vitisho takriban kila siku wa kutaka kuupinduwa kwa nguvu utawala wa kikatiba wa Cuba.

Hali ya mitaa ya Havana kufuatia matatizo makubwa ya kiuchumi
Hali ya mitaa ya Havana kufuatia matatizo makubwa ya kiuchumiPicha: Norlys Perez/REUTERS

Majivu ya Fidel Castro kusafirishwa Santiago

Na mtizamo huo wa Marekani ndio kitu pekee ambacho kinaonesha uhalisia wa  vita vikali vya kibiashara inavyovifanya dhidi ya Cuba kuuadhibu umma wote wa taifa hilo.

Hivi sasa Cuba inakabiliwa na tatizo kubwa la umeme na rais Donald Trumpkwa wiki kadhaa amekuwa akirudia kauli moja tu kwamba taifa hilo liko ukingoni kuporomoka kabisa. Washington imeongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Cuba, ikilenga kuikatia uwezo wa kuingiza fedha ya kigeni na mafuta.

Shinikizo hilo lilishika kasi baada ya utawala huo wa Trump kuendesha operesheni kubwa ya kijeshi mnamo mwezi Januari ya kumkamata rais aliyekuwa madarakani nchini Venezuela Nicolas Maduro, kutoka mjini Caracas na kusafirisha hadi Marekani.

Hatua hiyo iliiondolea Havana mmoja ya washirika wake muhimu kabisa ambaye amekuwa kwa miaka akiiunga mkono Cuba, na hasa kwa kuisadia kuipatia mafuta kutokana na nchi hiyo kuwa chini ya vikwazo vya kibiashara kwa miongo ilivyowekewa na  Marekani.

Rais Donald Trump amekuwa akitowa vitisho vya kuitwaa kwa nguvu Cuba.
Rais Donald Trump amekuwa akitowa vitisho vya kuitwaa kwa nguvu Cuba. Picha: Pablo Porciuncula/Saul Loeb/AFP

Kwa sasa Cuba ni moja ya mataifa yanayopitia wakati mgumu kabisa wa hali mbaya ya migogoro ya kiuchumi ambayo haijapata kuonekana tangu mapinduzi yaliyoongozwa na Fidel Castro mnamo mwaka 1959.

Cuba na Marekani: Marafiki walio na nyuso mbili

Jana ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa ilizungumzia wasiwasi wake kuhusu hali ya ukosefu wa mafuta inayoikumba Cuba ambayo imesababisha matatizo mbali mbali nchini humo.Msemaji wa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa,Farhan Haq, Jana Jumanne alifafanua kile kinachoendelea nchini humo.

"Wenzetu katika ofisi ya kuratibu shughuli za kiutu wametuambia kwamba wanazidi kuwa na wasiwasi kuona  ukosefu wa mafuta unazidi kuwafanya watu washindwe kuzifikia huduma muhimu kote nchini.Wenzetu wanatuambia kwamba kuna mirundo ya takataka zilizoshindwa kuondolewa katika mitaa ya mji wa Havana,na hali ya hewa imechafuka kutokana na uvundo wa kuchomwa kwa taka hizo na moshi wa kuni. Mamlaka pia zimeripoti kwamba katika mwezi Februari peke yake, wameshindwa kufanya upasuaji wa wagonjwa 50,000''

Cuba chini ya Diaz, imeimaliza enzi ya Catro iliyotawala  kwa tariban miaka 60
Cuba chini ya Diaz, imeimaliza enzi ya Catro iliyotawala kwa tariban miaka 60Picha: Eliana Aponte/dpa/picture alliance

Serikali mjini Havana iko kwenye hali ngumu sana ya shinikizo huku Washington ikitekeleza sera yake ya kuzidi kuitia kishindo Cuba ikizuia usafirishaji mafuta,na ikisema waziwazi kwamba inataka kuufikisha mwisho mvutano wa takriban miongo saba kati yake na taifa hilo ambalo limekuwa chini ya chama kimoja cha Kikomunisti.