Cuba na Marekani: Marafiki walio na nyuso mbili | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Cuba na Marekani: Marafiki walio na nyuso mbili

Baada ya kurejea kwa mahusiano ya kidiplomasia miaka 5 iliyopita, Cuba na Marekani bado hazipikwi chungu kimoja. Vikwazo vya Marekani sasa ni vikali zaidi kuliko wakati mwingine wowote

Ilikuwa ni rais Barack Obama aliyeanzisha enzi mpya ya mahusiano kati ya Marekani na Cuba. Rais huyo wa Marekani alizungumzia juu ya mwanzo mpya baada ya miongo chungunzima ya kutoaminiana baina ya mataifa hayo jirani.

Kwa kuanzia alitangaza kuondoa vizuizi vya kusafiri na pia kutoa ruhusa ya kurejea tena huduma za kutuma na kupokea fedha kati ya Washington na Havana

Mazungumzo ya kwanza kati ya wakuu wa nchi hizo mbili yalifanyika wakati wa mkutano wa kilele wa mataifa ya Amerika. Obama akaiondoa Cuba kutoka orodha ya Marekani ya mataifa yanayofadhili ugaidi na kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na hata akamtuma waziri wa mambo ya kigeni wakati huo John Kerry kwenda mjini Havana kufungua tena ubalozi wa Marekani.

Mwezi Machi mwaka 2016, Obama mwenyewe aliizuru Cuba kwa ziara ya siku tatu ambapo rais wa Cuba wakati huo Raul Castro alitoa wito wa kuondolewa vikwazo vyote vya kiuchumi dhidi ya nchi yake. Lakini hilo halikufanyika.

Baada ya hatua za mwendo wa konokono maendeleo yote hayo yakaanza kubadili mwelekeo - Novemba 8 mwaka 2016 wiki mbili kabla ya kifo cha kiongozi mwanamapinduzi wa Cuba Fidel Castro, Donald Trump akashinda urais wa Marekani na mara moja akaanza kubadili mkondo wa mahusiano kati ya Washington na Havana.

Kuba Proklamation der neuen Verfassung

Raul Castro (katikati) na Rais wa Cuba Miguel Diaz Canel

Hivi sasa Cuba imerejeshwa katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi na Marekani imeweka masharti mapya yanayofanya iwe vigumu kwa wacuba wanaoishi nchini humo kutuma pesa nyumbani kwao na pia imeweka vizuizi vya kupeleka mahitaji muhimu ya tiba katika kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.

Historia ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Cuba ilianza miaka 60 iliyopita kwa rais Dwight Eisenhower kuzuia uingizwaji wa sukari kutoka Cuba na kuwashauri raia wa Marekani kutosafiri kwenda Cuba.

Marekani ilifuta rasmi mahusiano yake ya kidiploamasi na Cuba, Januari, 3 mwaka 1961.

Marekani ilifikiri kuwa vikwazo hivyo vingemtikisa haraka sana Fidel Castro na wanamapinduzi wake. Lakini matarajio hayo yalikuwa ya kufikirika tu hakuna klichofanikiwa.

Tangu wakati huo ikawa ni mfululizo wa makabiliano makali kati ya mataifa hayo mawili. Akiwa madarakani rais John F. Kennedy alijikuta katika kisanga cha mpango wa mtangulizi wake wa kutumia kundi la wacuba walio uhamishoni kwa msaada wa shriika la kijasusi la Marekani CIA la kujaribu kumpindua rais Fidel Castro.

Operesheni hiyo ilipotekelezwa April 17, 1961 ilizimwa mara moja na vikois vya jeshi la Cuba. Mwaka mmoja baadae rais Kennedy aliwekea Cuba vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi. Oktoba 1962 mzozo kati ya Marekani na Cuba ulifikia kiwango cha kutisha na kukaribia kuutumbukiza ulimwengu katika vita vya silaha za nyuklia.

Kuba Noam Chomsky und Fidel Castro | 2003

Fidel Castro na Noam Chomsky(kulia) mjini Havana 2003

Hali hiyo ilichochewa na mpango wa uliokuwa muungano wa kisovieti wa kupeleka makombora ya nyuklia nchini Cuba.

Mivutano iliendelea kwa matukio chungunzima ya uhasama kati ya Washington na Havana hadi pale rais Jimmy Carter alipojaribu mwaka 1977 kuchukua hatua ndogo ya kulegeza marufuku ya kusafiri na kufungua ujumbe wa kidiplomasia wa Marekani nchini Cuba.

Muongo mmoja baadae uzani wa nguvu duniani ukabadilika. Ukuta wa Berlin uliangushwa, vita baridi ikafunga pazia lake na mtetezi mkuu wa Cuba, uliokuwa Muungano wa kisovieti ukaparaganyika.

Cuba ikatumbukia katika kipindi kigumu sana. Mgao wa umeme ukawa wa kila wakati, bidhaa muhimu hazikuwa zikipatikana tena na uchumi wa taifa ulianguka kwa karibu asilimia 50 kati ya mwaka 1989 hadi 1992.

 Viongozi wa Marekani wa zama hizo Ronald Reagan na mrithi wake George H.W. Bush wote waliaendeleza hatua kali ya vikwazo na mbinyo dhidi ya Cuba.

Rais Bill Clinton kwa upande wake alijaribu kutuliza mivutano lakini mrithi wake George W. Bush aliendeleza sera ya hatua kali dhidi ya Cuba.

Wakati mrithi wa Fidel ambaye ni mdogo wake Raul Castro waliporejesha mahusiano ya kidiploamisa na rais Obama walinyanyua bendera ya matumaini. Lakini kusema kweli mafanikio yote yaliyopatikana yamerudishwa nyuma mno na rais wa sasa Donald Trump.