1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yatafuta amani Afrika kwa uwekezaji

15 Oktoba 2012

China hivi karibuni inaweza kutanuwa harakati zake za kiuchumi barani Afrika kwa kujihusisha katika masuala ya amani na usalama barani humo, kwa mujibu wa Mkutano wa Ushauri kati ya China na Afrika uliofanyika Ethiopia.

https://p.dw.com/p/16QCp
Wafanyakazi wa ujenzi wa China barani Afrika.
Wafanyakazi wa ujenzi wa China barani Afrika.Picha: Getty Images

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Amani na Usalama nchini Ethiopia, Mulugeta Gebrehiwol, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba hakuna kitu ambacho kisichoguswa na amani na usalama aidha uwe unatafuta ushirikiano wa uwekezaji, shughuli za kiuchumi au kitu chochote kile. Amesema hiyo ni zana kuu yenye kuweka mazingira ya maingiliano na ushirikiano.

Maafisa waandamizi wa serikali na wasomi mashuhuri akiwemo Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, Demeke Mekkonnen, na makamo wa rais wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Kigeni, Profesa Zhu Liqun, walihudhuria mkutano huo uliofanyika Bishoftu kama kilomita 45 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa.

Maafisa wa serikali ya China wamesema sera ya taifa hilo kubwa la Bara la Asia la kutoingilia kati masuala ya Afrika isitafsiriwe kuwa ni sawa na kutojali masuala ya amani na usalama wa bara hilo

China yashikilia kutokuingilia mambo ya ndani ya Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema sera yao ya kutoingilia kati masuala ya Afrika haimaanishi kwamba hawayajali masuala ya Afrika. Amesema wanapinga kisingizio kinachotumiwa na baadhi ya nchi cha kujali masuala ya Afrika kwa kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi za bara hilo.

Wafanyakazi wa ujenzi wa China barani Afrika.
Wafanyakazi wa ujenzi wa China barani Afrika.Picha: Getty Images

Hadi sasa dhima ya China barani Afrika kwa kiasi kikubwa ilikuwa imejikita katika maendeleo ya kiuchumi.Takwimu kutoka Wizara ya Biashara ya China zinaonyesha kwamba hapo mwaka jana biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola bilioni 166.

Kwa mujibu wa wataalamu msimamo wa China wa kutoingilia kati masuala ya ndani ya Afrika umepelekea bara hilo kujipatia misaada ya fedha inayoihitaji mno bila ya kuwekewa masharti ambayo baadhi ya mataifa ya magharibi huyaweka wakati wa kutowa mikopo kwa Afrika. Msimamo huo wa China umechangia ujenzi wa haraka wa miradi ya miundo mbinu barani humo.

China imejikita kwenye miradi mikubwa ya ujenzi

Kwa mujibu wa utafiti juu ya dhima ya China katika shughuli za ujenzi katika maendeleo ya miundo mbinu barani Afrika, kampuni za China hivi sasa zinahodhi sekta ya ujenzi barani humo ambapo fungu lake katika soko ni kubwa kuliko yale ya Ufaransa, Italia na Marekani yakichanganywa kwa pamoja.

Rais Jacob Zuma wa Afika ya Kusini (kushoto) akikaribishwa na Rais Hu Jintao wa China katika mkutano wa Afrika na China, Beijing tarehe 19 Julai 2012.
Rais Jacob Zuma wa Afika ya Kusini (kushoto) akikaribishwa na Rais Hu Jintao wa China katika mkutano wa Afrika na China, Beijing tarehe 19 Julai 2012.Picha: dapd

Mapato ya kampuni zake za ujenzi huko Afrika ya kati na kusini mwa Afrika yameongezeka sana halikadhalika hisa zake katika soko la Afrika.

Taasisi za fedha za taifa nchini China kama vile Benki ya Exim ya China na Benki ya Maendeleo ya China zimekuwa wakopeshaji wakubwa barani Afrika kwa kushindana na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuhusiana na fedha za msaada wa maendeleo.

Mambo mengi yameandikwa juu ya mikopo ya Benki ya Dunia na IMF kwa Afrika. Kutokana na taasisi hizo mbili kutumia msaada wao kushinikiza kwa nchi maskini sera za mageuzi ya kiuchumi kama vile ubinafsishaji na kuregeza masharti ya biashara masharti hayo nchini Mali yamepelekea kupanda kwa gharama za umeme ambazo yumkini zikiwatahiri wakulima wa pamba pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa misaada.

China kuwekeza dola bilioni 20 Afrika

Rais Hu Jintao wa China alitangaza miezi miwili iliyopita kwamba nchi yake itawekeza dola bilioni 20 zaidi barani Afrika. Pia alisema kwamba China itachukua hatua mpya kusaidia harakati za amani na maendeleo barani Afrika. Sera tayari zimekuwa zikiandaliwa kuashiria jinsi China itakavyoboresha ushiriki wake.

Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa China na Afrika, Beijing tarehe 19 Julai 2012.
Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa China na Afrika, Beijing tarehe 19 Julai 2012.Picha: dapd

Lakini dhima ya China barani Afrika mara nyingi imekuwa ikionekana kuwa na utata.Hatua ya China kugharamia ujenzi wa makao makuu mapya ya Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Addis Ababa imezusha mdahalo miongoni mwa watu wasioikosowa Afrika iwapo China inajipenyeza barani Afrika.

Mataifa ya magharibi yameonya mara kadhaa kwamba kushiriki kwa China barani Afrika kuna dahamira za kikoloni. Au kuunga mkono tawala za ukandamizaji na kujaribu kufaidika na rasilmali za bara la Afrika.

Hata hivyo Dr. Mehari Taddele Maru mtaalamu wa kujitegemea wa amani na usalama katika mada yake ya Uhusiano wa China na Afrka : Maeneo ya Mageuzi Ushirika Endelevu hakubaliani na tuhuma hizo kwa kusema kwamba sifa ya China barani Afrika ni nzuri kwani nchi za Afrika zinahisi kwamba mshirika wao huyo wa Asia anaheshimu watu wengine, utamaduni na mataifa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Mohammed Khelef